MFUMO WA ELIMU UNAOZALISHA VILAZA


                  Neno kilaza si neno geni masikioni mwa wengi.Neno hili limetokea kijizolea umaarufu zaidi miongoni mwa watanzania siku chache zilozopita tangu kufukuzwa kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma chuo kikuu cha dodoma.Kwa mujibu wa rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania,wanafunzi wale waliondolewa   chuoni kwa kutokidhi vigezo vya kusoma Elimu ya Chuo kikuu.
            Kwa kifupi neno kilaza linaweza
kutafsiriwa kama mbumbu,kichwa maji,boya,n.k,ilimradi liwe na maana ya mtu asiyeweza kupata/kusomea kiwango flan cha elimu.Au yule anayefanya kinyume na matarajio.
             Tangu kutokea kwa lile tukio pale Dodoma.Nimekuwa nikifuatilia mijadala na chambuzi mbalimbali kutoka kwa wadau tofauti walioguswa na tukio lile.Nikiwa nazidi kutafakari kwa kina kuhusiana na neno kilaza.Ghafla nashtushwa na taarifa zilizoandikwa katika gazeti la jambo Leo 9/8/2016."61% YA WAHITIMU WA CHUO KIKUU TANZANIA NI VILAZA"
          Nikiwa kama mmoja wa wadau wa elimu hapa nchini niliguswa na taarifa hizo.Pia nilipata mkanganyiko kidogo wa kiakili kuhusiana na maana kamili ya neno kilaza au vilaza.Nikajiuliza wale wanafunzi walitimuliwa pale udom kwa kukosa sifa za wao kusoma Chuo kikuu(vilaza).Nikashangaa tena!wapo waliofaulu wakajiunga hatimaye wakahitimu katika ngazi mbalimbali kama stashahada,shahada,shahada za uzamili na uzamivu nakuendelea.Leo utafiti unafanyika tunaambiwa 61% Kati ya wahitimu hao hawana tija kwa taifa,yaani hawafiti katika nyanja mbalimbali za ujenzi wa taifa(vilaza).
       61% Ina maana kama wahitimu ni 100 basi 61 hawatoshi(vilaza),kama ni 1000 basi 610 wapo katika kundi hilo.
             Nikajaribu kuwafananisha wale waliokosa vigezo na wale waliohitimu lakini hawana tija kwa taifa.Nikajiuliza je hawa wanatofauti gani.Kama wale walikosa sifa tukawaita vilaza,je hawa 61% kwanini wasiitwe vilaza pia.Ingawa sidhani  kama ni jina sahihi kuwaita vijana wetu wenye sifa hizo. Sidhani kama kutowaita hivyo ni sahihi pia.Kwa tafsri ya walio wengi neno hili linatumika kumaanisha walioshindwa na wasioweza.
             Katika jamii yeyote ile iliyostarabika haiwezi kujivunia kuwa na kizazi cha vilaza.Pia ni aibu na fedheha kushabikia jambo kama hilo kwani ni hatari kwa maslahi ya nchi na taifa kwa ujumla.
             Nilijiuliza je  chanzo cha yote haya ni nini hasa?Je ni shule na vyuo vyetu ndio tatizo kwa maana Elimu itolewayo haikidhi.Je ni walimu wanaofundisha au ni wanafunzi wenyewe?Yote haya yanaweza kuwa chanzo kwa namna moja au nyingine.Je katika hili ni nani wa kulaumiwa?
           Hapo ndipo niliona umuhimu wa kutazama mfumo mzima wa elimu yetu.Inawezekana kabisa mfumo wa elimu tulionao ndio chanzo cha kutengeneza kizazi cha vilaza.
            Tunapotazama mfumo wa elimu katika Tanzania.Tunarudi nyuma kidogo hadi kipindi kile cha ukoloni.Elimu iliotolewa kipindi cha ukoloni haikuwa na lengo mahususi la kumnufaisha Mtanzania,Bali kumjenga kuwa mzalishaji mzuri na mnyenyekevu kwa wakoloni.Ilikuwa ni elimu ya kibaguzi kwa maana ya rangi,matabaka na jinsia,kwani ni wachache walioweza kupata Elimu hii hususani watoto wa machifu tena wakiume pekee(African history,19c to 21C A.D,Stephen James).Hivyo Elimu ile ilichangia kwa kiasi kikubwa kimrudisha nyuma Mtanzania kimaendeleo(Walter Rodney -how Europe underdeveloped Africa)
              Pia elimu ile kwa kiasi flan ilichangia kuwafungua kifkra waafrica wachache ambao walipigania haki na usawa,hatimaye tukapata uhuru,mfano mwl.Julius kambarage Nyerere.
               Mwaka 1961 Tanganyika iliungana na baadhi ya nchi za kiafrica kama Ghana ambazo zilijitangazia uhuru wao kutoka makucha ya wakoloni.
             Mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuzaa nchi ilioitwa Tanzania.
               Mapema  mwanzoni mwa mwaka  1967 Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mwl.Nyerere alitangaza Azimio la Arusha.Azimio hilo lilikuwa na sera za kuleta usawa,umoja na kuondoa kila aina ya uonevu toka kwa wakoloni(rejea kitabu Azimio la Arusha).
              Pia ilitangazwa sera ya "Ujamaa na kujitegemea"kama njia bora ya kumuongoza Mtanzania katika kumletea maendeleo
            Elimu haikupewa mgongo kwani mwl.aliweka Sera na mfumo mzuri katika elimu ya Tanzania.
               Elimu ya kujitegemea na elimu ya watu wazima ziliwekwa na kupewa kipaumbele.Kwa ufupi Elimu ya watu wazima ililenga kumuwezesha Mtanzania mtu mzima kujua kusoma na kuandika,kuondoa ujinga na kuwa makini/sambamba na hali halisi ya kisiasa iliokuwepo(kitabu sera ya elimu ya kujitegemea 1967 kimeeleza kiundani).Kupitia elimu ile Watanzania wengi watu wazima waliweza kujipatia maarifa yaliyo wajenga kifikra na kujitambua.
           Elimu ya kujitegemea ni ile iliokuwa kwenye mfumo maalum.Ilijumuisha elimu ya msingi,sekondari na elimu ya juu.Ni elimu iliolenga kumjenga mwanafunzi kifikra,kisaikolojia,ufundi na ujuzi mbalimbali kivitendo.Kama sera ya ujamaa na kujitegemea ilivyokuwa.Elimu ile pia ilikusudia kumjenga muhitimu aweze kujitegemea katika nyanja zote kama uchumi,siasa,jamii na utamaduni.Kwani walijifunza kusoma na kuandika,ufundi,kilimo,ufugaji n.k.
       Elimu ya msingi ilijitosheleza kwani muhitimu alimaliza akiwa na maarifa na ujuzi mbalimbali kuweza kujitegemea hata kama akuendelea na sekondari.Mitihani ilikuwepo ili kumpa umakini mwanafunzi na si kupima ukilaza.Elimu ile iliwajenga Watanzania kuwa wazalendo wa nchi yao,utamaduni wao,kujiamini na kujitegemea.Kwa waliosoma Enzi hizo ni mashahidi wa hilo.
        Tanzania ya Leo imefanikiwa kuwa na shule za msingi na sekondari katika ngazi zote(Mkoa,wilaya,Tarafa,kata na vijiji).Pia vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu vimejaa chungu Tele kila kona ya nchi.
         Je ni wapi tulipokosea?kwanini kuwepo na ongezeko la vilaza?kama tulivyoona wale ambao hawakidhi viwango vya ufaulu kwenda Chuo kikuu wanaitwa vilaza.Wale wanaokidhi vigezo wakihitimu wengi wao ni vilaza.!Je mitihani ni kipimo sahihi cha kutambua ukilaza wa mwanafunzi?
         Unapotazama mfumo wa elimu yetu kwa sasa.Haufanani kabisa na mfumo wa elimu uliokuwepo tangu nchi imepata uhuru mpaka mwishoni mwa miaka ya themanini(kujiamini,kujitambua,usawa na kujitegemea).
         Elimu yetu kwa sasa inavijitambia kama vya elimu ile ya kikolono(ubaguzi,kutojiamini na utegemezi)
        Mwl Nyerere alikuwa na ndoto ya kuona Tanzania ni nchi huru inayojitegemea.Aliweka juhudi pia za kufanya KISWAHILI kuwa lugha ya kufundishi na kujifunzia mashuleni(msingi hadi Chuo kikuu-Azimio la Arusha).
          Ingawa ndoto hizo hazikufikiwa kwa wakati.Bado haiwezi kubadili ukweli kwamba kosa kubwa tunaloendelea kulifanya katika elimu,Ni kuendelea kutumia lugha mbili katika utoaji wa elimu.Hapa nazungumzia kingereza na kiswahili.
             Shule zote za sekondari na vyuo vikuu nchini vinatumia kingereza kama lugha ya kufundishia na mawasiliano.Shule zote za msingi zinazomilikiwa na serikali zinatumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia na mawasiliano shuleni.Wakati huohuo shule zinazomilikiwa na taasisi na watu binafsi zinatumia kingereza kama lugha ya kufundishia na mawasiliano(English medium).
           Shule zote hizo zina lengo moja la kumpatia mwanafunzi maarifa.Ukitazama hapo utaona ubaguzi na matabaka katika elimu.Wanafunzi wengi wanaosoma katika shule za watu na taasisi binafsi wengi wao wanatoka katika familia zenye uwezo kifedha.Shule za serikali kwa kiasi kikubwa zinahudumia wanafunzi kutoka familia za kimaskini na zile za kawaida Sana.
          Wanafunzi hawa wanapofanikiwa kwenda sekondari utofauti Mkubwa unajitokeza.Kwakuwa shule za sekondari zinatumia kingereza kama lugha ya kufundishia na kujifunzia.Unafuu pia unajitokeza kwa wale waliosoma shule za msingi za binafsi,kwasababu inakuwa nafuu kwa wao kuendeleza maarifa waliyopata shule ya msingi.Kwa wanafunzi waliosoma shule za msingi za serikali wanajikuta wanaanza upya Elimu kwani kila kitu kinabadilika.Inawapasa waanze kujifunza lugha ya kingereza ili waweze kumudu masomo yao.
           Kwa kiasi kikubwa wale waliosoma shule binafsi(English medium)wanakuwa na nafasi kubwa Sana ya kuelewa kile kinachofundishwa.Wengi wanaofanya vizuri sekondari kwa waliosoma shule za msingi za serikali ni wale wenye uwezo/upeo Mkubwa wa kukariri.
          Wanafunzi wengi wanaofaulu vizuri katika mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari(form four na form six)ni wale kutoka shule za binafsi.Ambazo ukichunguza kwa makini ni shule zile zilozokusanya wanafunzi wengi toka shule za msingi za binafsi(English medium).Shule ambazo kwa kiasi kikubwa wanafunzi kutoka familia za kawaida na maskini hawawezi kuzimudu.Wanafunzi wengi katika kundi hili ndio wale tunaosikia wapo kwenye kumi bora ya wanafunzi waliofaulu vizuri kila mwaka
           Ukichnguza kwa makini katika wahitimu wa Chuo kikuu.61% ya vilaza wanaosemwa kwa kiasi kikubwa imekusanya wengi kutoka wale waliosoma shule za msingi za serikali.
           Kwa kifupi mfumo huu wa elimu ndio unaotengeneza wahitimu wasiojiamini,wasiojikubali na wasioweza kujitegemea.Leo katika Tanzania mtu yule anayeweza kutumia lugha ya kingereza(kuongea na kuandika)ndiye anayeonekana msomi halisi.
          Mfumo huu pia umeleta matabaka Kati ya wanafunzi hawa waliosoma elimu ileile katika lugha  tofauti.
           Mfumo huu pia umezalisha wahitimu/wasomi wasioweza kujitegemea.Kwani wengi wao walikariri vitu kuliko kuelewa,hivyo wamegeuka tegemezi.Mfano wapo mainjinia wengi Sana kutoka vyuo mbalimbali lakini miundombinu kama barabara,madaraja,majengo makubwa mfano jengo la bunge,yanatengenezwa na mainjinia toka nchi za nje kama,china,ulaya n.k.
           Kuna matabibu wengi Sana hapa nchini ila hakuna kificho kwamba tiba za uhakika zinapatikana India,Marekani ,Africa kusini n.k.
           Elimu imejenga jamii isiyojikubali.Mfano ukitembelea maeneo ya vijijini katika Tanzania ambako watu wengi kiswahili bado kinawasumbua,kingereza ndio shida kabisa.Lakini sio jambo geni kukuta vitu kama Mazengo pub,Maganga shop,Ngosha saloon n.k.Wengi hawapendi kutumia lugha Mama kwani elimu imefanya lugha asili ionekane haifai.
          Elimu imeijenga jamii Ione kiswahili ni lugha isiyo na hisia.Hata kama mtu hajui kingereza.Ni nadra Sana kuwasikia wenzi wakiitana mpenzi wangu bali my love au baby au dear n.k
           Ukiendelea kuchunguza kwa undani utagundua tatizo kubwa ni lugha.Kwa mfano nchi nyingi duniani zilizoendelea kiuchumi,siasa,jamiii na utamaduni ni zile zinazotumia lugha mama katika elimu na mawasiliano,mfano Japan,China,Korea,Tailand,Uingereza,Ufaransa,Italia,Na nyingine nyingi Sana.
           Fikra sahihi huja kwa lugha sahihi(Mrisho mporo-mwanafasihi)
         Mfano nenda maeneo ya Rufiji au kilwa.Kawaulize baadhi ya vijana waliopata daraja 0 katika mitihani yao,wakupe historia ya vita vya majimaji kwa lugha ya kiswahili.Utashangaa watakusimulia na watakupa mifano thabiti pengine mwl Wako pale st.Francis sekondari hakuwahi kuvijua!Vijana wale walipata 0 si kwamba hawajui vita vya majimaji.Bali walishindwa kueleza "causes and effects of majimaji uprising".
           Halikadhalika nenda Unguja na Pemba ambako Mara nyingi tunasikia shule zao zimekuwa zikishika nafasi za mwisho katika mitihani.Kawaulize wale vijana waliofeli wakupe historia ya sultan said seyyid.Naamini vitu watakavyokupa mwl Wako wa historia pale Feza sekondari havifahamu.Vijana wale walifeli kwa sababu walishindwa kueleza,(why sultan said seyyid shifted his capital from Muscat to Zanzibar?"
             Hiyo ni baadhi tu ya mifano inayotupa picha ni jinsi gani tutaondokana na tatizo la vilaza.Kumbe tatizo hapo sio vilaza,kilaza bali ni LUGHA.
          Kama tutataka kufika pale tunapotamani kufika yatupasa safari hiyo ianze Leo.Hoja za miaka mingi ni kwamba KISWAHILI ni lugha yenye misamiati michache ya kisayansi,hivyo hakiwezi kutumika katika elimu kufundishia na mawasiliano(shule za msingi hadi Chuo kikuu).Yatupasa tutambue kuwa lugha yeyote ile inaendelea kukua kadri inavyozidi kutumika Mara kwa Mara.Mfano kingereza kilichozungumzwa mwaka 1910 ni tofauti na kingereza kinachozungumzwa Leo.Kingereza cha Leo kimekua na kuongeza misamiati mingi ya kukopa toka lugha mbalimbali.Hivyo basi kiswahili pia kitakua kama kitaanza kutumika katika nyanja mbalimbali za elimu.(msingi hadi Chuo kikuu)
            Nachukua nafasi hii kuipongeza serikali ya awamu ya tano.Kwa kuamua kutoa Elimu bure kuanzia shule za msingi na sekondari zote za serikali(kidato cha kwanza hadi cha nne).Pia kwa kufanya jitihada za kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati.
         Mwanafalsafa  Maria Montessori aliwahi kupendekeza  ili kujenga uelewa mzuri kwa mwanafunzi.Ni vema kufanya chumba cha kusomea(darasa)kuwa sehemu vutivu,mfano kuwa na madawati mazuri,picha mbalimbali,maua n.k ili kufanya darasa kuwa sehemu huru.
            Tukumbuke kuwa hata kama tutaweka viti vya kuzunguka na masofa darasani.Pasipo kulitazama suala la LUGHA bado tutaendelea kuzalisha kizazi cha vilaza.
  

 Imeandikwa na Jijo masta the black gene.

Chapisha Maoni

0 Maoni