ACT-Wazalendo wasuka njama za kuivuruga CCM Mbarali.

BAADHI ya wanachama wa ACT-Wazalendo wilayani Mbarali, wanatajwa kusuka njama za kuhujumu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutengeneza tuhuma dhidi ya mbunge wa jimbo hilo Haroon Mulla na kuzisambaza mitandaoni.
Taarifa zinamtaja Dk. Anthony Mwandulami aliyekuwa meneja wa kampeni wa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Dickson Kilufi kuwa ndiye anayesuka mipango hiyo ili kumchafua kisiasa mbunge huyo. Kwa mujibu wa mawasiliano yaliyonaswa, Dk.Mwandulami ambaye pia ni mfanyabiashara na mganga wa kienyeji, amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na ujangiri Robert Mande na inaelezwa ni kumpa taarifa za mbunge huyo, ambapo mawasiliano ya karibuni ni 24, Oktoba majira ya saa 1:06 jioni, ambapo walizungumza kwa dakika 281. Taarifa zaidi zinasema, wakati huo ambao Mwandulami akiwasiliana na Mande, askari wa kikosi cha kupambana na ujangili walikuwa kwenye shamba la uwekezaji la mbunge huyo wakichimba kile kinachodaiwa ni kutafuta meno ya tembo yanayaodaiwa kufukiwa shambani hapo. Inaelezwa askari hao hawakufanikiwa kukuta meno ya tembo na badala yake kwenye upekuzi wao walikuta nyama ya swala ambayo ilihifadhiwa baada ya wahusika kuwinda kwa kutumia kibali walichonacho.

Hata hivyo, askari hao walichukua nyama hiyo na kudai ni nyara ya serikali ambapo baadaye mtoto wa mbunge huyo anayeitwa Fahad Pirmohamed, anayesimamia shamba hilo alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Milioni 138 ambayo walilipa na kuachiwa huru. “Kuna jambo lipo nyuma ya kesi hii na kilichopo ni siasa tena za kuchafuana, Dk.Mwandulami alimpigia kampeni Kilufi, wakashindwa na wameenda kukata rufaa mahakamani dhidi ya Haroon Mulla, wakati kesi inaendelea, kunaibuka madai ya mbunge kuhusika na meno ya tembo na kinachotia mashaka zaidi siku moja kabla ya kesi ya kupinga ubunge kuanza kusikilizwa, usiku zinasambazwa taarifa kwamba mbunge anahusishwa na ujangiri na kweli kwake kulipekuliwa” alisema mtoa taarifa ambaye ni mkazi wa Mbarali. Aidha, mwananchi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema anachofanya Dk. Mwandulami ni kucheza siasa za majitaka ili kuhakikisha heshima ya mbunge huyo inashuka na ikibidi kumuondolea uhalali wa kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo ili kumpa nafasi Kilufi aliyeshindwa akiwa CCM, akahamia Chadema ambako alikosa nafasi ya kuteuliwa kugombea ubunge na kuhamia ACT aliposhindwa ubunge. “Mchezo mbaya zaidi anaofanya Dk. Mwandulami ni kupeleka taarifa za uongo hata kwa waziri Maghembe (Waziri wa Maliasili na Utalii) na hata ukiangalia kuna mawasiliano walifanya Oktoba 23 saa nne usiku na walizungumza kwa dakika 19, sasa Waziri naye amedanganywa, TANAPA nao wameingizwa mkenge na kutumika kwenye mchezo huu wa kisiasa” alisema mtoa taarifa huyo. Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa, tayari baadhi ya vyombo vya habari likiwemo gazeti la Mtanzania ambalo liliripoti habari hiyo, wamebaini mchezo huo wa kisiasa na tayari wamemuomba radhi mbunge Haroon Mulla huku taarifa za ndani kwenye Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakisita kutoa ufafanuzi wa suala hilo baada ya kubaini vita za kisiasa kwenye suala hilo. “Hadi leo TANAPA wapo kimya, walisema watatoa taarifa juu ya suala hilo lakini wanasita maana wamegundua kuna siasa zinachezwa na kuna upotoshwaji unafanywa na mtu ambaye ana malengo yake binafsi, nashauri viongozi wetu wawe makini maana kuna upotoshwaji mkubwa unaendelea kwenye suala hili”    

Chapisha Maoni

0 Maoni