Kizimbani kwa kumnyanyasa na kumfanyia ukatili mtoto wake huko Sengerema

Mwanamke mmoja wilayani Sengerema mkoani Mwanza amekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumfanyia ukatili mtoto mdogo wa mwaka mmoja na miezi miwili.


Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza imemtaja mwanamke huyo kuwa ni Rhoda Juma mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa kijiji cha kilabela wilayani humo, ambaye anadaiwa kumfungia ndani ya nyumba kwa muda wa miezi minne na kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili mtoto huyo wa kike aitwaye juliana kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa akiishi na mtoto huyo hapo nyumbani kwake baada ya kuletewa na rafiki yake aliyejulikana kwa jina moja la Rahel ambaye inadaiwa ndiye mama mzazi wa mtoto huyo, na kwenda kusikojulikana katika shughuli zake za uhudumu wa baa.
Aidha inadaiwa kuwa kwa kipindi chote cha miezi minne mtoto alikuwa akifungiwa ndani na kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea mtoto kuwa na makovu mengi mwilini na kudhoofika kiafya,

Majirani walimuona mtoto huyo wakati mama mwenye kaya alipokwenda kwenye shughuli zake na kuacha mlango wazi ndipo walitoa taarifa polisi na kusaidia mtuhumiwa kukamatwa.
Mtoto huyo amelazwa hospitali ya wilaya ya Sengerema akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Chapisha Maoni

0 Maoni