Uhuru na umoja ni ngao ya utaifa wetu

Leo hii nimepata muda wa kutafakari nguvu au uzito wa maneno yanayopatikana katika wimbo wa taifa letu. Muktadha mkubwa katika wimbo huu ni maombi kwa Mungu kuibariki Afrika hali kadhalika kuibariki Tanzania. 

Kuna ombi la kuomba kwa Muumba alete baraka kwa viongozi, maombi ya kuomba hekima, umoja na amani kama ngao kwetu Waafrika na watu wake.
Sehemu ya pili ni maombi tena kwa Mungu aibariki Tanzania, inafuatiwa na kumsihi Alie juu kudumisha uhuru na umoja kwa wanawake, wanaume na watoto.
Kibwagizo cha wimbo wa Taifa kimejikita kuomba baraka kwa Afrika, Tanzania na baraka kwa watoto wa Afrika vilevile baraka kwa watoto wa Tanzania.
Naomba msomaji wa makala hii ujikite katika kutafakari uzito wa maneo yenye dua kwa Muumba wa mbingu nan chi adumieshe uhuru na umoja ukiwa ni msingi wa ulinzi wetu. Tukumbuke ngao ni moja ya silaha za kijadi toka nyakati za kale ambazo wazee wetu walishika kujilinda dhidi ya mashambulizi ya mikuki au mishale iliyokuwa inarushwa na maadui kwa nia ya kuwadhuru au kuwaua kabisa. Lengo la kushika ngao kwa mpigananji ni kujikinga dhidi ya mishale, mkuki au silaha yoyte inaoweza kuondoa uhai au kuleta majeraha makubwa katika mwili wa mshika ngao.
Tukiwa tumetimiza miaka 55 ya uhuru na miaka 54 ya Jamhuri, ni vema tukatafakari kwa pamoja na kwa kina, kwa marefu, kwa ,apana hali kadhalika kwa kimo; je, sisi Watanzania bado tunajiona wamoja dhidi ya maadui zetu wa ndani nan je ya mipaka yetu?
Wanaume, wanawake na watoto tunahusika kujenga Tanzania kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa la Tanzania kwa sisi tulio ndani ya mipaka ya nchi hii na kwa walio nje ya nchi. Utaifa wetu unakuwa na nguvu sana pale ambapo UMOJA unakuwa na nguvu kubwa bila kujali kama mimi naishi kijijini Nyamatala wilayani Kwimba au kama wewe msoji uko Atlanta, nchini Marekani.
Rai yangu ni kuwa umoja na amani ni silaha wa kujilinda dhidi ya maadui hali kadhalika ni silaha za kutuunganisha ili tusonga mbele kimaendeleo kama famila ya akina baba, akina mama na watoto.
Wimbo wa Taifa umejikita kutamka baraka kwa viongozi wetu. Dhamana ya kutuogoza tumeiweka kwao kuanzia ngazi ya wenyeviti wa vitongoji kwa serikali za mtaa mpaka ngazi ya kitaifa inayoongozwa na Mheshimiwa Rais na ambae ni mkuu wa nchi na kiongozi wa mhimili wa utawala (executie branch) ambae ana wasaidizi kupitia baraza la mawaziri, wakuu wa mikoa, wiliaya mpaka ngazi ya tarafa . Je, tunatamka nini kwa viongozi wetu, lawama kwa changamoto wanazozipitia au kuwashauri kwa nia njema ili kutuongoza vyema?
Kwa wale tunapata fursa ya kwemda kwenye nyumba za ibada tutakuwa tumewahi kusoma hekima za mfalme Sulemani mwandishi wa kitabu cha methali. Mfalme Sulemani amenukuliwa akisema mauti na uzima upo katika nguvu ya ulimi na kwa wale wanaoupenda watakula matunda yake.
Jambo jema la kutia moyo ni kuwa viongozi wengi wa kitaifa wenye nafasi ya kutuunganisha waliapa kwa kushika vitabu vya dini ambazo zina amini kwenye kutuunganisha kama jamii ya amani dhidi ya chuki. Je, sisi tulio na nafasi ya kuongoza, tunatamka nini kama viongozi, hayo tunayonena ni baraka kwa taifa hili au kinyume chake? Tuliopa ee Mungu nisaidie, tuliomba msaada wa kutuunganisha ile tusonge mbele, au hata hatukumbuki kama tuliomba msaaada kwa Alie juu?
Ni maombi yangu turejee upya uzito wa mistari ya wimbo wa Taifa wa kuomba baraka na kuwabariki viongozi wetu kama msingi wa umoja na amani yetu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Tanzania tunayoitaka. 
Mungu ibariki Tanzania, Wabariki viongozi wetu

Chapisha Maoni

0 Maoni