Mizengo Pinda alia na viongozi wala rushwa


Na Paul Mabeja, Dodoma
WAZIRI mkuu mstaafu katika serikali ya awanu ya nne, Mizengo Pinda, amewataka viongozi katika ngazi mbalimbali kuwa waadilifu badala ya kuwa wabinafsi, waeneza chuki na wala rushwa.


Rai hiyo aliitoa jana alipokuwa akifunga kongamano la Maombi ya kuliombea taifa pamoja na viongozi mbalimbali ndani ya serikali.

Alisema kuwa ili uweze kuwa na taifa lenye viongozi wazuri wasihojihusisha katika vitendo vya rushwa na kuwa na utawala bora ni lazima kupata viongozi ambao ni wacha Mungu na wenye hofu.

Pinda alisema viongozi ndani ya serikali, kwenye vyama vya siasa pamoja na Taasisi mbalimbali lazima wafanye kazi zao kwa hofu ya Mungu kutoka moyoni na siyo maigiizo, ili waweze kuwapatia wananchi maendeleo.

"Viongozi kama watafanya kazi zao kwa uadilifu ni wazi kuwa kila mwananchi ataweza kujivunia na kujiongezea kipato kutokana na rasilimali zinazotokana na vyanzo mbalimbali ambavyo Mungu ameviweka katika nchi yetu" alisema Pinda.

Vilevile Pinda alisema kuna haja ya kuanzishwa kwa vikundi vya maombi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kuweka njia bora ambayo watoto watakuwa waaminifu katika utendaji wao wa kazi kwa misingi ya kujitenga na ufisadi, rushwa pamoja na ubadhilifu wa mali za Umma.

Naye kiongozi aliyekuwa makamu wa benki ya dunia kanda ya Afrika Dk.Oby Ezekwesili kutoka nchini Nigeria akitoa mada katika kongamano la maombi juu ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji alisema kuwa ili nchi iweze kusonga mbele ni lazima kuwa na viongozi ambao wanazingatia misingi ya utawala bora.

Pia Dk. Ezekwesili alihimiza uongozi ambao unazingatia masuala ya utekelezaji wa demokrasia, uwazi, uwajibikaji pamoja na utawala bora ili kila mmoja aweze kujivunia rasilimali za nchi.

Aidha kiongozi huyo alisisitiza utoaji wa elimu juu ya kutunza Maliasili za nchi huku suala zima la uzalishaji likipewa kipaumbele kwa njia ya kutunza vyanzo vyote vya mapato ikiwa ni pamoja na kujiepusha na masuala ya rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali za Umma.

Chapisha Maoni

0 Maoni