SIASA ZA TANZANIA NA USALITI WA VIONGOZI KWA WAPIGA KURA

Aghalabu, kumekuwepo na wimbi kubwa la usaliti wa wanasiasa kwa wapiga kura wao hasa wanapokalia viti walivyokuwa wakivitaka, na kabla ya kuvikalia, huwa wapo tayari hata kupiga magoti kwa wapiga kura ili hal tu
wawapigie kura.

Itakumbukwa siku Mh. JPM alipokuwa akifungua kampeni katika viwanja vya  jangwani huku akitumia takribani dakika 53 kueleza sera na vipaumbele 25 vyake kama ahadi kwa watanzania. Mbali na hayo yote, naomba nijikite kwenye ahadi moja tu ambayo, licha ya kuwa inanigusa mimi na watoto wengine wa wakulima, yeye pia aliizungumza kwa mhemko na hisia kali ambazo ziliamsha hisia za maelfu ya watoto wa maskini ambao walihisi wamepata mkombozi wa kweli.

Watoto wa maskini kutengwa kwenye utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Si kutengwa tu, bali pia, kwa masikio yangu mwenyewe nilimsikia mheshimiwa akigusa hadi tatizo la kucheleweshwa kwa mikopo kwa wanafunzi wanapodahiliwa kujiunga na elimu ya juu. '...kwanza umeambiwa kitu kinaitwa mkopo, halafu tena unamcheleweshea mkopaji, hiiii, nene yaya gete...' alisema Mhe. JPM. Hapo ndipo nilijikuta nikisimama bila kujua nimesimamaje huku machozi yakinilengalenga na kuniaminisha kuwa hakika ukombozi wa mtoto wa kitanzania ndiyo umefika haswa! Masalale! Kumbe nilisahau kuwa, nilichokuwa naangalia kilikuwa ni siasa na mbio za kukifuata kiti kule magogoni!

Usaliti waanza. Iwe siri yangu ya matokeo yangu ya kushangilia kipaumbele kile, na hivyo nisizungumzie sana nini kilitokea katika udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2015/2016, badalal yake hebu tuangalie kwa mfano hai wa sasa ambao unaonekana dhahili bila hata ya kuambiwa tazama. Kati ya wanafunzi 58,000, serikali ina mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 24,000 tu, idadi ambayo kusema kweli haifiki hata nusu wa wanafunzi wote. Kwa sasa, ni wanafunzi 3960 tu ndiyo wapo kwenye 'allocation' ya mkopo katika batch ya kwanza ya bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB). Swali ni je, yawezekana kweli rais wangu kasahau kabisa ahadi hii?

Serikali pia imetangaza vipaumbele katika udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kuwa, fani za tiba, wahandisi na walimu katika masomo ya sayansi na hisabati ndiyo watakaopata mkopo kwa kipaumbele cha hali ya juu. Swali ni je, hawa wanafunzi walioorodheshwa kwenye kipaumbele cha mwaka huu wenyewe wanapewa mikopo kwa kodi inayolipwa na nani kama si mlala hoi?

Ushauri wangu: wanafunzi wapewe mikopo kutokana na uhitaji wao, na washauri wa mkuu wamshauri kuwa, watanzania hawa maskini wamewekeza kwenye elimu ambayo wanaamini ndiyo pekee itawakwamua katika maisha yao.

Mwisho kabisa niiombe wizara yenye dhamana ijichunguze kwanza kuwa, kuanzia mkuu mwenyewe alisoma kwa kodi ya nani pale UDSM? Lakini pia, waziri mwenye dhamana yeye alisoma kwa pesa ipi? Nafikiri huo utakuwa ni mfano kwao ili kujua kwamba, alichowafanyia Mwl Nyerere kilikuwa ni deni ambalo sasa wanatakiwa kulilipa kwa watoto wa kilala hoi leo.

Chapisha Maoni

0 Maoni