WAZIRI SIMBACHAWENE AMUUNGA MKONO DC HAPI TASAF

WAZIRI SIMBACHAWENE AMUUNGA MKONO DC HAPI TASAF

** AAGIZA FEDHA ZA TASAF ZILIZOLIWA ZIREJESHWE

**WARATIBU TASAF WASIMAMISHWE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene ameziagiza Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa katika Mpango wa kunusuru kaya maskini unaofanywa kwa uratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) kurejeshwa ili ziweze kuwanufaisha walengwa.

Mhe. Simbachawene pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasimamisha kazi Waratibu wote wa TASAF wilaya ili kufanya uchunguzi wa jinsi walivyojihusisha katika kuvuruga utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini kwa kuandikisha kaya zisizokuwa na sifa na ametaka wale wote watakaobainika kuhusika katika kutenda makosa mamlaka za kinidhamu kuchukua hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma leo tarehe 25/11/2016, Mhe. Simbachawene amesema usimamizi dhaifu wa mpango wa TASAF katika ngazi za halmashauri hususani Waratibu wa Mpango wa TASAF Wilaya wasiokuwa waaminifu katika kutekeleza majukumu yao imesababisha fedha za Mpango wa TASAF kutumiwa na watu wasiokuwa walengwa.

Waziri Simbachawene pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuwachukulia hatua watumishi wa ngazi za Kata, Mitaa na Vijiji ambao kwa namna moja au nyingine watabainika kuhusika katika kuvuruga Mpango wa kuzinusuru kaya maskini kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Aidha, Mhe. Simbachawene amewataka Wakuu wa Mikoa kujiridhisha katika mikoa yao ikiwa Wakurugenzi watachukua hatua stahiki dhidi ya watumishi wasiokuwa waaminifu na kuwataka kumpelekea taarifa hiyo ndani ya siku kumi na nne kuanzia leo tarehe 25/11/2016.

Mheshimiwa Simbachawene ameitaja mikoa inayoongoza kwa matumizi mabaya ya fedha za Mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF kuwa ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro, , Shinyanga, Arusha, Kigoma, Dodoma, Arusha na Mbeya.

Ikumbukwe kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi mwanzoni mwa wiki hii tarehe 22/11/2016 akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake aliagiza kuvuliwa madaraka kwa Mratibu wa TASAF wilaya ya Kinondoni kutokana na ufisadi katika fedha za TASAF.

Aidha, Hapi aliagiza vyombo vya dola kuanza uchunguzi mara moja na wahusika wote kufikishwa kwenye vyombo vya sheria huku fedha zilizopewa kwa wasio na sifa kurejeshwa mara moja.
Kinondoni inakua wilaya ya kwanza kuwa tayari imeshatekeleza agizo la Waziri Simbachawene kabla ya kutolewa kwake.

Chapisha Maoni

0 Maoni