Kocha wa Simba asema hawako salama

Pamoja na Simba SC kujihakikishia kuwa kwa vyovyote vile itakavyokuwa itaumaliza mwaka 2016 ikiwa kileleni huku ikiongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya watani zao, Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, amesisitiza hawako salama kwamba wanaweza kupumzika sasa.


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Hans Pluijm, naye amesema kuwa wao wana kibarua kigumu zaidi ya Simba.


Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru ulitosha kuipaisha Simba kwa kuongeza pengo la pointi kwa kufikisha jumla ya pointi 41, dhidi ya 37 za Yanga ambayo Ijumaa ililazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon.

Omog anaamini kufuatwa kwa karibu na Yanga siyo ‘mazingira rafiki’, badala yake tageti yake anapata unafuu iwapo watakuwa mbele zaidi ya pointi hizo kwani ni chache na mambo yanaweza kubadilika muda wowote.

“Nafarijika kuona tupo kileleni lakini bado huwezi kusema tuko sehemu salama. Pointi nne hazitoshi, ni kidogo sana kwa timu kama Yanga. Tunatakiwa kufanya kazi zaidi na zaidi kuhakikisha tunajiweka katika mazingira mazuri,” alisema Omog.


Naye Pluijm alisema: “Kwa ubora wa timu, ukweli mpaka sasa Yanga bado ndiyo timu bora japo tulishindwa kupata ushindi kwenye mchezo uliyopita (Lyon), lakini kwa suala la tofauti ya pointi nne, kweli kunatakiwa kufanya kazi zaidi kuhakikisha tunabaki kwenye mbio za ubingwa. Tunahitaji kufanyia kazi kila kosa kwa timu nzima ambalo kimsingi kwa sasa lipo mikononi mwa kocha mkuu (George Lwandamina).”

Chapisha Maoni

0 Maoni