Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, ametaka vijana wa chama hicho kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia aliodai unafanywa na watawala.
Alisema hayo juzi alipokutana na vijana wa chama hicho ambao ni wanavyuo (CHASO) wa vyuo vikuu mkoani hapa.
Lowassa ambaye yuko Tabora kwa ziara ya kuimarisha chama, aliwataka vijana hao kuwa na ujasiri wa kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia kwani vijana duniani ndio chachu ya mabadiliko.
“Nimekuja Tabora kuwashukuru kwa kura nyingi mlizonipigia na hamasa kubwa mliyoionesha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Katika uchaguzi ule tulishinda, lakini ushindi mkubwa zaidi ni tulipofanikiwa kuvumilia na kuweka maslahi ya watoto, wazee na mama zetu mbele,"alisema na kuongeza:
"Amani ni tunu muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa kuliko kitu kingine chochote. Msikate tamaa, tumejipanga vema kwa uchaguzi ujao wa mwaka 2020 na hatutadhulumiwa tena haki yetu, kama ilivyokuwa mwaka jana,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema Jambo Kuu na la msingi ambalo wana Chadema wanatakiwa kuwa nalo sasa katika chama ni umoja na mshikamano kati yao.
"Umuhimu wa umoja na mshikamano ndani ya chama chetu ni mkubwa sana, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inajaribu kwa kila namna kukandamiza Upinzani na demokrasia na jambo hili si geni, ukirudi nyuma katika historia ya vyama vya siasa nchini, hata kabla ya Uhuru, unaweza kuona umoja ulivyoisadia TANU dhidi ya chokochoko za chama alichoanzisha mkoloni wakati ule - United Tanganyika Party (UTP) kukabiliana na kuidhoofisha TANU na kumzuia Mwafrika kupata Uhuru na kujitawala," alisema.
Aliwaambia vijana kwamba changamoto kama hizo ni za kawaida kwa vyama vingi vya upinzani hasa Afrika, ambavyo vinaungwa mkono na wananchi wengi wakiamini ni vya ukombozi.
Lakini pia alisema katika kujenga umoja na mshikamano huo ndani ya chama, ni lazima nguvu kubwa ipelekwe kwenye matawi waliko wananchi.
"Katika chama chochote cha siasa watu wengi hawako ngazi za juu, bali mashinani. Ni lazima nguvu yetu kubwa ielekezwe huko kwa sasa, ili kuhakikisha chama kinakuwa na misingi madhubuti ambayo inaweza kutumika kukisaidia nyakati za uchaguzi," alisema.
Aidha, Lowassa ambaye katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana alipata asilimia 38 ya kura, alihoji umuhimu wa Serikali kununua ndege zaidi, kuliko kupeleka huduma muhimu vijijini.
"Tumesikia nia njema yao ya kuagiza ndege nyingine zaidi miaka miwili ijayo, lakini tunajiuliza, je isingekuwa busara kutumia fedha hizo kupeleka maji safi na salama mijini na vijijini?" Alihoji.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA