News alert: Tanesco yatimiza agizo la serikali la kumpatia umeme Bakhresa


SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetimiza agizo la Rais John Magufuli la kukipatia umeme kiwanda cha kusindika matunda cha Azam Fruits Processing Plant, mali ya mfanyabishara, Said Salim Bakhresa kabla ya muda wa miezi miwili waliyopewa kukamilisha kazi hiyo.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo Oktoba 6, mwaka huu alipokuwa anazindua kiwanda hicho kilichopo Mwandege, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani kufuatia kilio kilichotolewa na uongozi wa kiwanda hicho kuiomba serikali iingilie kati ili kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji bidhaa kiwandani hapo.

“Tayari tumetimiza agizo la Rais la kukipatia umeme kiwanda cha Bakhresa, Mkuranga Novemba 30, mwaka huu kwa kufikisha umeme kiwandani hapo,” Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alitoa maelezo hayo jana jijini Dar es Salaam.

Mramba alikuwa anatoa majumuisho kwa wahariri wa vyombo vya habari baada ya ziara ya kutembelea miradi ya ukarabati wa miundombinu ya usambazaji umeme jijini Dar es Salaam.

Alifafanua umeme umefikishwa kiwandani hapo na kilichobaki ni upande wa kiwanda chenyewe ambao unasubiri baadhi ya vifaa kutoka nje ili waweze kuingiza umeme ndani ya kiwanda.

Alisema Tanesco inajenga njia tatu za umeme kuelekea Mkuranga na mbili kati hizo ni kwa ajili ya viwanda vipya wilayani humo na moja kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Katika juhudi za kuboresha miundombinu ya Tanesco ili kukidhi adhma ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa viwanda, shirika lake linatekeleza miradi ya ukarabati wa miundo mbinu ya umeme kwa nchi nzima itakayogharimu Sh zaidi ya trilioni 5.4.

Alifafanua miradi hiyo ni pamoja na uzalishaji, usafirishaji na vituo vya kusambazia umeme ambavyo mifumo ya zamani ya analogia inabadilishwa na kuwekwa mifumo mipya ya ya kisasa ya dijitali yenye ufanisi mzuri zaidi.

Vituo vya usambazaji umeme vya Dar es Salaam vilivyotembelewa vikiwa bado vinaendelea na ukarabati wa mifumo ya zamani na kuweka ya kisasa ni pamoja na Muhimbili, City Center, Sokoine na Kituo cha Ilala.

Chapisha Maoni

0 Maoni