Simba yarejea kileleni ligi kuu bara


SIMBA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Ndanda FC jioni ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara


Ushindi huo, unaifanya Simba ifikishe pointi 38 baada ya kucheza mechi 16, ikiwazidi kwa pointi mbili mabingwa watetezi, Yanga. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na Ahmed Kikumbo aliyesaidiwa na Josephat Bulali na Mohamed Mkono, dakika 45 za kwanza zilimalizika bila mabao.

Kiungo mpya wa Simba James Kotei kutoka Ghana alilazimika kumpisha Muzamil Yassin dakika ya 19 baada ya kuumia kufuatia kugongana na Nahodha wa Ndanda, Kiggi Makasi.

Muzamil Yassin ameseti bao moja na kufunga moja Simba ikishinda 2-0 Mtwara leo

Kipa Mghana wa Simba alifanya kazi ya ziada dakika ya 20 kumzuia mshambuliaji chipukizi wa Ndanda, Riffat Khamis asifunge baada ya kufanikiwa kuwatoka mabeki.

Dakika saba kabla ya mapumziko, mshambuliaji wa Simba Ibrahim Hajib alipiga shuti zuri la mpira wa adhabu ambalo liliupita ukuta wa Ndanda, lakini likatoka nje sentimita chache. 

Kipindi cha pili, Ndanda ilipata pigo dakika ya 52 baada ya beki wake Hemd Khoja kuumia na kushindwa kuendela na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Benito John.

Pengo la Khoja lilionekana wazi kuiathiri Ndanda, kwani baada ya hapo Simba wakaanza kuipenya ngome ya wenyeji wao kwa urahisi na kupata mabao mawili.

Mshambuliaji Muivory Coast wa Simba, Frederick Blagnon hakuamini macho yake dakika 59 baada ya mpira wa kichwa alioupiga kuunganisha krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuokolewa vizuri na kipa Jeremiah Kasubi.

Dakika moja baadaye, winga Shizza Kichuya akamdakisha kipa Kasubi shuti dhaifu la karibu ndani ya sita kufuatia pasi ya Mo Ibrahim.

Hatimaye Muzamil Yassin akaifungia Simba bao la kwanza kwa shuti kali dakika ya 63 akimalizia pasi ya Mo Ibrahim.

Baada ya bao hilo, Ndanda walionekana kupoteana na kuwaruhusu Simba kuuteka zaidi mchezo.
Hata hivyo. kuanzia dakika ya 80, Ndanda walitulia kidogo, ingawa Simba waliendelea kutawala mchezo.

Mo Ibrahim akaifungia Simba bao la pili dakika ya 91 akimalizia pasi ya kiufundi ya Muzamil.
Mechi nyingine za leo African Lyon imetoa sare ya 0-0 na Azam FC, Mbao FC imeilaza 1-0 Stand United na Mbeya wenyeji Prisons wameifunga 1-0 Maji Maji.

Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa; Jeremiah Kisubi, Kiggi Makassy, Bakari Mtama, Paul Ngalema, Hemed Khoja/Benito John dk53, Salvatory Ntebe, Nassor Kapama, Salum Minelly, Salum Telela, Omar Mponda/Helbert Lukindo dk77 na Riffat Khamisi.

Chapisha Maoni

0 Maoni