Januari 21, 2015, nilipata kuandika yafuatayo kwenye ukurasa wangu wa Facebeook;
"Afrika changamoto kubwa ya marais walioingia madarakani wakiwa vijana sana, kama Joseph Kabila ( DRC) ,Yahya Jammeh ( Gambia) na Blaise Compaore ( Burkina Faso), ni ukweli, kuwa huwa na hofu ya kwenda kuishi maisha ya nje ya Ikulu wakiwa hata hawajafikisha miaka 50, na kwamba huwa na hofu ya mfumo mpya utakaokuja nyuma yao kuja kuwashughulikia.
Kwao, njia pekee ya kuepuka wanayoyahofia, ni kubaki madarakani, kwa udi na uvumba!
Inasikitisha."
Ndugu zangu, Tumemwona Joseph Kabila anavyoweweseka juu ya namna atakavyoishi maisha ya nje ya Ikulu, tarehe za Uchaguzi zinabadilishwa mara kwa mara. Tumemwona sasa Yahya Jammeh anavyoweweseka. Ndicho hiki nilichokiona, na hakika sikuhitaji kuwa na elimu ya unajimu kuyaona hayo.
Majuzi hapa nimehojiwa na mtangazaji kijana wa redio moja hapa nchini mwetu. Nikiwa kama mwanahabari nguli, kwa alivyonitambulisha huyo mtangazaji mwenyewe, alitaka kujua maoni yangu juu ya nchi zetu za Kiafrika kujitoa kwenye Mahakama Ya Kimataifa Ya Uhalifu Wa Kivita ( ICC).
Nilimjibu, kuwa inahitajika sana. Kwamba yumkini viongozi wa Kiafrika wenye kutenda maovu kwa watu wao, na hata wapinzani wao kisiasa, hamwogopi Mungu, bali wanaiogopa sana ICC.
Leo Afrika kuna Marais wenye kuhofia kuamrisha mauaji kwa wenye kuwapinga, si kwa hofu ya Mungu, bali ICC. Ni ukweli wenye kusikitisha.
Na kwa yanayotokea Gambia, ni aibu ya Jammeh, ni aibu ya Afrika pia. Ni aibu yetu sote.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA