Vijana wanaotoka katika halmashauri za wilaya ya Kahama Mji,Ushetu,Msalala na Manispaa ya Shinyanga wamekutana katika bonanza la michezo lililoandaliwa na Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI.
Bonanza hilo la michezo limejumuisha vijana 150 wenye umri kati ya miaka 14-19 wanaotoka katika klabu za vijana zilizoundwa na zinasimamiwa na shirika la AGPAHI kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya husika.
Akifungua bonanza hilo katika uwanja wa taifa mjini Kahama leo Jumamosi Desemba 17,2016,mgeni rasmi Dr. Anthony Kasomelo kutoka hospitali ya mji wa Kahama,alisema bonanza hilo ni kwa ajili ya vijana kufurahi,kufahamiana,kupata marafiki wapya,kuonyesha vipaji na kujifunza.
"Vijana hawa wanatoka kwenye vikundi 12 vilivyopo katika halmashauri nne za mkoa wa shinyanga,ambazo ni Msalala,Kahama mji,Ushetu na manispaa ya Shinyanga", alisema Kasomelo.
Dr. Kasomelo alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika la AGPAHI kwa kuendelea kuwa karibu na vijana huku akiwaasa vijana hao kuendelea kuwa wafuasi wazuri wa huduma za afya ili kuboresha afya zao ili waweze kutimiza ndoto zao.
Aidha alitoa wito kwa viongozi wa halmashauri za wilaya kuendelea kutoa ushirikiano kwa shirika la AGPAHI hasa katika kutekeleza majukumu ya kuwasaidia wananchi katika huduma za afya hususani kwa watu wanaopata tiba na matunzo ili huduma zipatikane katika ubora na ziwe rafiki kwa wananchi.
Awali akizungumza katika bonanza hilo, Afisa mradi wa watoto kutoka Shirika la AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Jane Kashumba alisema wafadhili wa bonanza hilo ni shirika la Uingereza linalofadhili huduma za kuboresha maisha ya watoto (Children's Investment Fund Foundation -CIFF).
Kashumba alibainisha kuwa shirika la AGPAHI limeanzisha klabu 12 za vijana zenye wastani wa vijana 20 - 70 walio katika rika balehe.
"Lengo la vikundi hivi ni kuwakutanisha vijana kila mwezi ili waweze kujifunza pamoja masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya msukumo rika kwa vijana,kushirikiana katika kutatua changamoto zao na njia za kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi vijana hao wameendelea kunufaika na elimu hiyo",alieleza Kashumba.
Miongoni mwa michezo iliyochezwa na vijana hao ni pamoja mpira wa miguu,kuvuta Kamba,mbio za magunia,kukimbiza kuku ,kuimba nyimbo na kucheza muziki ambapo washindi waliibuka na zawadi mbalimbali.
Bonanza hilo limehudhuriwa na wadhibiti wa Ukimwi kutoka halmashauri za wilaya,wasimamizi wa klabu za vijana,wafanyakazi wa shirika la AGPAHI na wadau mbalimbali wa michezo na mambo ya afya.
Angalia matukio katika picha yaliyojiri uwanjani hapa chini
Afisa mradi wa watoto kutoka Shirika la AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Jane Kashumba akizungumza wakati Bonanza la michezo katika uwanja wa taifa wa mjini Kahama
Mgeni rasmi Dr. Anthony Kasomelo kutoka hospitali ya mji wa Kahama akifungua bonanza hilo la vijana lililokutanisha vijana 150 ambapo mbali na kulipongeza shirika la AGPAHI alitumia fursa hiyo kuwaasa vijana hao kupenda shule
Katikati ni mgeni rasmi Dr. Anthony Kasomelo akizungumza wakati wa kufungua bonanza la michezo.Kushoto ni Mhudumu wa jamii pia Afisa tabibu kutoka kituo cha afya cha Kolandoto katika manispaa ya Shinyanga Maryciana Bruno ,aliyeinama kulia ni Mganga mfawidhi zahanati ya Segese Denis Ngatale
Mgeni rasmi Dr. Anthony Kasomelo akiteta jambo na Jane Kashumba
Timu ya mpira wa miguu kutoka halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wakijiandaa kuanza mchezo baina yao na timu kutoka halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Msalala na Kahama Mji.
Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu kutoka manispaa ya Shinyanga wakiwa na walezi wao na maafisa kutoka AGPAHI
Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu kutoka halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Msalala na Kahama Mji wakipiga picha kabla ya mchezo
Wachezaji wa timu ya halmashauri ya wilaya ya Kahama Mji,Ushetu na Msalala wakiwa na walezi wao na maafisa kutoka AGPAHI
Dawati la ufundi timu ya Kahama Mji,Ushetu na Msalala
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA