Hatimaye kimeleeweka, hivi ndivyo utakavyoweza kutamka baada ya uongozi wa Yanga kuwalipa wachezaji wake mshahara na posho zao za mechi za Ligi Kuu Bara walizocheza.
Hiyo imekuja siku chache baada ya wachezaji hao kugomea mazoezi ya timu hiyo kwa siku mbili mfululizo, wakidai mshahara wa Novemba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo, wachezaji hao walilipwa mshahara na posho hizo juzi Ijumaa.
“Hakuna mchezaji yeyote anayeidai Yanga, kwa kifupi wachezaji wote wamelipwa mishahara sambamba na posho za mechi mbili walizokuwa wanazidai.
“Kikubwa kilichokwamisha wachezaji kulipwa kwa wakati ni mfumo uliobadilika katika malipo hayo, lakini kila kitu kilikuwa kipo vizuri, hivyo wachezaji wanachotakiwa hivi sasa ni kufanya kazi yao ndani ya uwanja.
“Kama uongozi tumejipanga vema kuhakikisha kuwa tatizo hili lililojitokeza halitajitokeza tena kwenye timu yetu, hivyo tumeandaa utaratibu mzuri wa malipo hayo,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Meneja Mkuu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, kuzungumzia hilo, alisema: “Kila kitu kipo vizuri kwenye timu, kwa maana ya malipo ya mshahara wao wa mwezi Novemba ambao wamelipwa.
“Hivyo, hakuna mchezaji yeyote anayedai mshahara katika timu na kitu kikubwa kilichobaki ni wachezaji kutimiza majukumu yao ya uwanjani.”
Nahodha Mkuu wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro', alilithibitisha hilo kwa kusema: “Hakuna mchezaji anayedai mshahara katika timu, wachezaji wote tumelipwa mshahara wetu wa mwezi Novemba.”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA