Idadi ya Watanzania wanaorudishwa kutoka nchi ya Msumbiji walikokuwa wakiishi, imezidi kuongezeka na kufikia 180 huku kukiwa na madai ya kuwafanyia vitendo vya kikatili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Uhamiaji mkoani Mtwara, Rose Mhagama alisema taarifa ambazo wamezipata hadi sasa ni kwamba bado Watanzania wengi wamefungiwa katika mahabusu za nchini humo na wanarudishwa kwa makundi.
Mhagama alisema sababu za kurudishwa kwa Watanzania hao bado hazijafahamika ila uchunguzi wa kina unaonyesha kwamba katika maeneo ya Mtepweshi na Nanyupu nchini humo, kuna migodi ya madini inayomilikiwa na raia kutoka moja ya nchi za Magharibi, anayedaiwa kufadhili askari wa nchi hiyo kuwafukuza Watanzania.
“Sijui ni kwanini na sifikirii sana kwamba Watanzania pekee ndio wapo kwenye maeneo hayo, kimsingi taarifa ambazo tunazo ni kwamba anaona kama Watanzania ndio wanakwenda kupora zile mali zilizopo katika machimbo hayo.
“Kiukweli zoezi hili linaleta sintofahamu nyingi kwa sababu unajiuliza kama kweli ni zoezi rasmi, kwanini wanawachania hati zao za kusafiria na kuwanyang’anya vitu vyao, inaonyesha wana nia ya kuwapora Watanzania mali zao au kutowatendea haki,” alisema.
Wakati ofisa hiyo akisema idadi ya Watanzania waliofukuzwa Msumbiji ni 180, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba amesema idadi ni watu 132 na ikitarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na operesheni ya kuwarudisha nyumbani wahamiaji haramu.
Alisema Februari 11, Watanzania 58 walirudishwa nchini kutoka Msumbiji, Februari 14 walirudishwa Watanzania 24 na jana walirudishwa wengine 50 ikiwa ni mwendelezo wa operesheni hiyo inayoendelea nchini humo.
Akizungumzia suala hilo jana jijini Dar es Salaam, Dk Kolimba alisema operesheni hiyo haijawalenga Watanzania pekee bali pia raia wa nchi nyingine walioingia Msumbiji kinyume cha taratibu.
Dk Kolimba alisema operesheni hiyo inaendeshwa katika mji wa Monte Puez uliopo Jimbo la Cabo Delgado na mji huo una Watanzania 3,000 wanaoishi huko na kwamba idadi ya watakaoondolewa huko inaweza kuongezeka zaidi.
“Tunaendelea kufuatilia tuhuma za baadhi ya Watanzania kwamba walifanyiwa ukatili wakati wanarudishwa nyumbani ili tujue hatua za kuchukua. Ubalozi wetu unashirikiana na serikali ya Msumbiji katika kuhakikisha Watanzania hawapati matatizo katika operesheni hiyo,”alisema Dk Kolimba.
Dk Kolimba alisema Serikali inaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao. Hata hivyo, alisisitiza kwamba uhusiano wa Tanzania na Msumbiji ni mzuri.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA