Rapa Nikki Mbishi leo kupitia mtandao wake wa Instgram aliweka ujumbe ukionyesha wimbo wake wa 'I'm sorry JK' kuwa umepigwa marufuku na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), jambo ambalo limeonesha kumgusa mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
"Baada ya salamu naomba niombe radhi kwa vyombo vyote vya habari kuwa sitoweza kuwapa ushirikiano wowote kuhusu wimbo wangu wa "I'M SORRY JK" uliositishwa na hii ni kwa usalama wao na wangu pia. Napokea simu nyingi sana zikihitaji maelezo juu ya suala hilo ila kiukweli kwa watakaohitaji taarifa kamili wanaweza kufika ofisi za BASATA, naomba nisiwe msemaji tena juu ya jambo hili" aliandika Niki Mbishi
Kutokana na sakata hilo Zitto Kabwe ameibuka na kuihoji serikali ya awamu ya tano kuwa inaogopa nini kiasi cha kuifungia kazi ya msanii huyo.
"Serikali imepiga marufuku wimbo wa msanii Nikki Mbishi. Wallah nilidhani ni utani kumbe kweli, serikali hii inachoogopa ni nini? Dah kua uyaone" aliandika Zitto Kabwe kupitia mtandao wake wa Twitter.
Mbali na hilo rapa Nikki Mbishi ameendelea kuwaomba watu wasiendelee kusambaza wimbo huo na kama wao watafanya hivyo basi yeye hatahusika katika suala hilo
"Kwa yeyote atakayeendelea kuusambaza au kuucheza popote pale mimi sitahusika naye maana 'technology' iko huru popote duniani na siwezi kuzuia watu wasiupate kwa kuwa ushasambaa, hivyo chukua tahadhari ili usijikute mikononi mwa sheria, naomba msubiri ujio wangu mpya wa singeli na aina nyingine za muziki kama naija, mchiriku" alisisitiza Nikki Mbishi
Katika ngoma hiyo, Nikki amejaribu kuonesha jinsi ambavyo alikosea kuukosoa utawala wa awamu ya nne, huku akikutana na hali ngumu zaidi katika utawala wa awamu ya tano, ambapo anafikisha ujumbe unaomaanisha kuwa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ulikuwa bora kuliko wa sasa.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA