Mbowe Aeleza Sababu za Chadema Kuamua Kumuunga Mkono Rais Kenyatta Uchaguzi Kenya.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ametangaza rasmi leo kuwa chama hicho kinamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu nchini Kenya.


Mbowe amesema kuwa uamuzi wa chama hicho kumuunga mkono umekuja baada ya kujiridhisha pasi na shaka kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Kenyatta, demokrasia imezidi kukua kwa kasi nchini Kenya.

Hayo yamesemwa na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani leo katika Mkutano Mkuu wa CHADEMA uliofanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na mamia ya viongozi wa chama kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Akieleza baadhi ya matukio yanayoashiria kukua kwa demokrasia nchini Kenya, Mbowe alisema kwa kipindi chote cha uongozi wa Kenyatta hakuna kiongozi yeyote wa kisiasa aliyewekwa kizuizini, mabadiliko ya katiba, bunge kuachwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na pia viongozi kuheshimu utawala wa sheria.

Baada ya tamko hili la CHADEMA kutolewa leo, baadhi ya watu wamelikosoa na kusema kuwa si sahihi kwa CHADEMA kumuunga mkono Kenyatta kwani akishinda na kuingia madarakani hatoweza kuwaunga CHADEMA mkono kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 kwa sababu za kidiplomasia.

Chapisha Maoni

0 Maoni