OMOG Ala Kiapo Kuisambaratisha Mbao Jumamosi..Adai Inyeshe Mvua Au Liwake Jua Lazima Wazikate Mbao


MECHI ya fainali ya Kombe la FA kati ya Simba na Mbao FC itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ni muhimu kuliko mechi nyingine zilizotangulia kwa sababu itaamua hatima ya klabu, wachezaji na benchi la ufundi, imeelezwa.

Mshindi wa mechi hiyo atakuwa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga wao watashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hapo mwakani.

Akizungumza  jana, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema kuwa katika kujiandaa na mchezo huo, kikosi chake kitaweka kambi ya siku mbili mkoani Morogoro na baadaye Alhamisi kitaelekea Dodoma tayari kwa mchezo huo.

Omog alisema ushindi ndiyo utawapa furaha na kuwafuta machozi Wanasimba wote ambao malengo yao ya kwanza yalikuwa ni kumaliza wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kabla ya msimu kumalizika.

"Ni mechi muhimu sana, tunahitaji ushindi, ushindi katika mchezo huo wa fainali ni muhimu kuliko kitu chochote kwetu, tunajua haitakuwa kazi rahisi kwa sababu hatutacheza peke yetu," alisema Omog.

Kocha huyo wa zamani wa Azam FC alisema wanaiheshimu Mbao na wataingia uwanjani wakijua wanakutana na moja ya timu zilizotoa ushindani na kuleta mabadiliko kwenye soka msimu huu.

Simba ilitinga fainali kwa mara ya kwanza baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC katika mechi ya hatua ya nusu fainali wakati Mbao FC iliyoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, yenyewe iliwavua ubingwa Yanga kutokana na kupata ushindi kama huo kupitia kwa beki wa Wanajangwani hao, Andrew Vicent 'Dante' aliyejifunga wakati akijitahidi kuokoa.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa tayari rufaa yao imeshafika katika makao makuu ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa) na kilichobakia ni wao kusubiri uamuzi utakaotolewa na shirikisho hilo.

Simba imepeleka malalamiko yake Fifa ikitaka kupewa pointi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambao walimchezesha Mohammed Fakhi anayedaiwa kuwa na kadi tatu za njano.

Chapisha Maoni

0 Maoni