Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika amefunguka na kumshauri Rais Magufuli jana bungeni na kusema Rais kabla ya kufikiria kuhusu makinikia alipaswa kufikiria kuhusu madini yanayochimbwa na kuchenjuliwa pasipo nchi kupata mapato.
Mnyika alisema hayo jana bungeni wakati akichangia katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo imewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18 ambapo Waziri aliomba bunge liweze kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 998. 3 ili kutekeleza majukumu yake katika wizara hiyo.
"Rais kabla ya kufikiria makinikia, angefikiria kuhusu madini yanayochimbwa na kuchenjuliwa kwa ukamilifu hapa nchini lakini nchi haipati mapato yanayostahili" alisema John Mnyika
Lakini pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Madini ya Nishati na Madini, Dotto Mashaka Biteko aliitaka serikali kufuta leseni zote za madini ambazo hazifuati sheria na zinakiuka sheria ya madini na hazijatekelezwa kwa muda mrefu ili wapewe wachimbaji wadogo wadogo.
"Leseni zote ambazo zinakiuka sheria ya madini ikiwa pamoja na kutotekelezwa kwa muda mrefu zifutwe na kupewa wachimbaji wadogo wadogo na wachimbaji wa kati kwa kuwa wameonyesha nia ya dhati ya kuendeleza sekta hiyo" alisema Biteko
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA