SERIKALI imewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanaondoa madarasa ya tembe, nyasi na udongo kwenye maeneo yao.
Pia amewaonya kuacha kutoa siri kwa kuwa kumekuwapo na tatizo kubwa la utunzaji wa siri za serikali na kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema hayo juzi alipokuwa akifungua awamu ya mwisho ya semina elekezi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Pwani na Mtwara, mjini hapa.
“Sitaki kuona madarasa ya tembe, udongo na nyasi na hili ni agizo kwa wakuu wa wilaya wote. Sitaki kuona na Mtwara ndiyo madarasa mengi yanaonekana ya nyasi, niwaombe wakuu wa wilaya hakikisheni mnasimamia halmashauri zenu hasa kwenye mapato ya ndani halmashauri nyingi hazipeleki fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Jafo.
Pia Aliwataka wakurugenzi hao kusimamia mapato yao ya ndani katika kujibu matatizo ya wananchi ikiwamo kuondoa madarasa hayo na watoto wanaosoma wakiwa nje.
"Niliona kupitia mitandao ya kijamii watoto wakiwa wamekaa nje wanasoma. Nikamtumia ujumbe mfupi mkuu wa wilaya wa Mtwara, sasa niwaagize wakuu wa wilaya na wakurugenzi sitaki kuona madarasa ya udongo au watoto wanakaa chini," alisema Jafo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA