WANANCHI wa Kata ya Inyeze wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamelalamika kwa diwani wa kata hiyo kwa kuvamiwa na kundi kubwa la fisi kijijini.
Hayo yamesemwa katika kikao cha baraza la madiwani na Diwani wa kata hiyo, Lucas Makulumo, ambaye alisema fisi hao wanaonekana muda wote wa mchana na usiku.
Diwani Makulumo alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abel Shija, aeleze halmashauri ina mpango gani juu ya wanyama hao waliovamia kata yake na kuhatarisha maisha ya wananchi wake.
Aidha diwani huyo alilieleza baraza hilo kuwa matukio ya wanyama hao kuvamia maeneo ya kata yake yamekuwa ya kawaida, hali inayowatia hofu wananchi wake, wakiwamo watoto wanakwenda shule. Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti Shija alisema alikubaliana na diwani huyo kuwa jambo hilo ni hatari na kuagiza hatua zichukuliwe mapema.
Alimuagiza mkurugenzi kuhakikisha anawatumia wataalamu wa maliasili na wanyamapori kuhakikisha wanyama hao kuondolewa na kuhakikisha hawaleti madhara kwa wananchi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA