KAMISHNA wa Operesheni wa Polisi (CP), Nsato Marijani amesema hadi sasa watuhumiwa waliokamatwa kudaiwa kuhusika na kifo cha Kada wa Chadema, Daniel John wamefikia wanne.
Pia amesema waliokamatwa katika tukio la kuuawa kwa kukatwa mapanga Diwani wa Kata ya Namwala Wilaya Kilombero, Geofrey Lwena wamefikia 10.
Amesema watuhumiwa wanaodaiwa kuandamana kinyume cha sheria na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini wamefikishwa mahakamani na uchunguzi unafanyika kwa aliyetenda.
CP Marijani ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam na kwamba upelelezi wa mauaji yote bado unaendelea.
"Kama tulishakamata watu wanne sisi tupo kwenye nafasi nzuri ya kusema nini kilikuwa sababu ya kifo hiki na nani waliokitenda, "amesema.
Amefafanua kuwa hawezi kuzungumzia zaidi kwani upelelezi unaendelea na kuwataka wananchi kuacha kusambaza taarifa ambazo hawana uhakika nazo.
Akizungumzia kifo cha Diwani Lwena, amesema wanataarifa zaidi za chanzo cha tukio hilo.
"Kadri upelelezi unavyoendelea tutajua wahusika wakina nani na tutawafikisha mahakamani,"amesema.Amesema vifo hivyo havihusiki na matukio ya kisiasa.
Akizungumzia maandamano, CP Marijani amesema jeshi la Polisi halitakubali kufanyika maandamano kwani ni kinyume cha sheria.
"Lolote linalofanyika katika nchi hii sisi kama jeshi la Polisi tunawaasa wananchi walifanye kwa mujibu wa sheria, suala la kufanya maandamano ukiwa na nia ya kuiondoa serikali ni uhaini, "amesema.
Amewataka wazazi na walezi wawaonye vijana wao kuwa vitendo wanavyokusudia kufanya ni uhaini na ni kinyume cha sheria.
"Ni dhahiri kwamba jeshi la Polisi haliwezi likakubali jambo hili litokee, tutafanya kila ambalo lipo kwenye uwezo wetu, kwa kadri tunavyoruhusiwa na sheria kuhakikisha kwamba jambo hili halifanyiki, "amesema na kuongeza;
"Sasa tusije baadae tukalaumiana, tumelisema hili wazi tunaamini kabisa watanzania waliokuwa wengi ni watu wazuri na wema wachache wasiotaka kufuata sheria na wanataka kuchezea usalama wa nchi hii basi sheria itachukua mkondo wake, "
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA