Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jana amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw. Li Yong.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa na lengo ya kujadiliana masuala mbalimbali ya uendelezaji Viwanda nchini Tanzania.
Mkurugenzi huyo amemjulisha Makamu wa Rais kuwa Tanzania ni nchi ya nne kuitembelea tangia ateuliwe .
Aidha katika mazungumzo hayo Mkurugenzi wa UNIDO amesema anajua Tanzania ajenda yao kuu ni uanzishwaji wa Viwanda na alimhakikishia Makamu wa Rais kwamba UNIDO itajitahidi kusaidia ajenda hiyo.
“Kuna umuhimu wa kuzingatia sekta binafsi na viwanda vidogo na vya kati wakati wa uanzishwaji viwanda ili vijana na wanawake wapate ajira,” alisema Mkurungenzi Mkuu wa UNIDO.
Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong amesema pia suala la uanzishwaji na Uendelezaji wa Viwanda ni lazima lizingatie masuala ya upatikanaji wa nishati na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha Mkurugenzi huyo alisifia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea ndani ya Serikali ya awamu ya tano na kusema UNIDO suala muhimu ni Utekelezaji.
Pia aliupongeza uongozi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na mashirikiano mazuri na Serikali.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alimhakikishia Mkurungenzi huyo wa UNIDO ushirikiano wa hali ya juu kutoka Serikalini na alimuomba kuipa Tanzania kipaumbele katika programu yake muhimu itakayochochea maendeleo ya Viwanda ya “Programmes For Country Partnership-PCP”.
Mwisho Kiongozi huyo aliishukuru Tanzania kwa mapokezi mazuri na programu nzuri walizompangia.
Viongozi wengine walioshiriki kwenye mazungumzo hayo ni Waziri wa Viwanda, Bishara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mgango pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Augustine Mahiga ambapo pia Waziri wa Viwanda , Biashara na Uwekezaji alitia saini pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong
Tamko la Kusudio la kuanzisha (Declaration of Intention) Mpango wa UNIDO unaojulikana kama “Programmes For Country Partnership-PCP” ambapo Makamu wa Rais alishuhudia kusainiwa kwa Tamko hilo,kusainiwa kwa tamko hilo kutarahisisha mchakato wa wa kukamilika kwa uwasilishwaji wa ombi la Tanzania kuomba iingizwe katika Mpango Maalumu wa UNIDO ambao ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya Viwanda.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA