Mamia ya watu wanaoishi na Virisi vya Ukimwi waacha kutumia ARVs


JUMLA ya  watu 456 wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi  katika Mkoa wa Simiyu ambao walioanzishiwa dawa za kufubaza  virusi (ARVs), wanadaiwa kuacha kutumia dawa hizo.


Idadi hiyo ni kati ya watu 1,669 wanaoishi na virusi vya Ukimwi katika mkoa huo ambao waliandikishwa kutumia dawa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2017 ambapo 1,213 (sawa na asilimia 73) ndio wanaondelea kutumia dawa.

Hayo yalisemwa na mratibu wa kudhibiti Ukimwi mkoa wa Simiyu, Dk. Khamis Kulemba, alipokuwa akifungua mafunzo kwa washauri na wafuatiliaji wa watu wenye VVU waliocha kutumia dawa yaliyokuwa yakitolewa na shirika la AGPAHI.

Kwa mujibu wa Dk. Kulemba, idadi hiyo ya wagonjwa ambayo ni sawa na asilimia 23 ya wagonjwa wote walianzishiwa dawa hizo, na wafuatiliaji hao hawajui waliko.

“Kuacha kutumia dawa kwa watu wenye VVU ni  hatari zaidi, kwani licha ya kutengeneza usugu wa vimelea kutokana na kutotumia dawa kwa  usahihi, pia inaweza kusababisha maambukizi mapya,” alisema Dk. Kulemba.

Mratibu huyo alisema lazima wagonjwa hao watafutwe popote walipo ili wapatiwe dawa na kuepusha hatari kubwa ya kuongezeka kwa wanaosihi na VVU.

Alisema kutokana na hali hiyo, Shirika la AGPAHI limeamua kusaidia katika mapambano hayo kwa kuwapatia mafunzo washauri ambao hutumika kuwatafuta na kuwashauri wagonjwa walioacha kutumia dawa.

“Ndiyo maana tumewaleta hapa na kuwapatia mafunzo, ni lazima hii asilimia 23 tuhakikishe wote wanapatikana na wanaanza kutumia dawa…katika mafunzo haya hakikisheni mnaweka mikakati ni kwa namna gani tutawapata,” alisema Dk. Kulemba.

Mratibu wa huduma unganishi kutoka AGPAHI, Herieth Novati, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha washauri hao wanafanya kazi yao kwa weledi na kuwarejesha ipasavyo wagonjwa waliocha dawa.

Chapisha Maoni

0 Maoni