Mwijage: Ni kweli cement imepanda hadi kufika 19,000 kwa mfuko ni kutokana na kiwanda cha Dangote kukosa umeme

saruji.jpg ​


Waziri wa viwanda, Charles Mwijage amesema kupanda kwa bei ya saruji kutoka 15,000 kwa mfuko hadi 19,000 baadhi ya maeneo imetokana na ukosefu wa umeme katika kiwanda cha Dangote Mtwara. Mhandisi wa umeme kanda ya kusini Azizi Salum amesema tatizo hilo la umeme mkoa wa lindi na Mtwara serikali imeagiza mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati 4.

======

Mtwara. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kupanda kwa bei ya saruji mkoani hapa kumesababishwa na kusimama kwa uzalishaji katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.

Upatikanaji wa saruji mkoani Mtwara umekuwa hafifu huku baadhi ya maduka ya vifaa vya ujenzi yakiwa yameishiwa bidhaa hiyo.

Hali hiyo imesababisha mfuko wa saruji kuuzwa kati ya Sh14,000 hadi Sh19,000 kutoka Sh10,500 hadi 12,000 kutegemea na eneo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri Mwijage alisema kwamba sababu nyingine ni kusuasua kwa uzalishaji katika Kiwanda cha Saruji cha Mtwara kilichokuwa na shida ya umeme na kwamba wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walikuwa wakiendelea na matengenezo ili kurusha huduma hiyo.

Waziri Mwijage alisema mtambo katika kiwanda cha Dangote uliharibika na kwamba wanategemea uzalishaji utarudi hivi karibuni baada ya kutengeneza. “Mtambo wa Kiwanda cha Dangote uliharibika walikuwa wanatengeneza hizo spea zake. Kutokana na kuadimika kwa saruji hiyo wafanyabiashara wanalazimika kuagiza kutoka Tanga na Dar es Salaam kwa hiyo ndiyo sababu tumerudi kwenye bei ya zamani lakini ni suala la muda umeme utarudi nina uhakika Dangote wataweza kulimaliza tatizo na kuanza uzalishaji siku nne zijazo,” alisema Mwijage.

Kuhusu suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika, Mhandisi wa Umeme Kanda ya Kusini, Azizi Salum alisema tatizo lipo kwa mkoa wa Lindi na Mtwara na kwamba tayari Serikali imeshaagiza mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati 4.

Alisema kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara chenye uwezo wa kuzalisha megawati 18, kwa sasa kinazalisha megawati 16 baada ya mashine moja kuharibika.

Chanzo: Mwananchi

Chapisha Maoni

0 Maoni