Ofisi ya Waziri Mkuu inapenda kuujulisha UMMA wa Watanzania kuwa kumekuwepo na taarifa zilizozua taharuki baina ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo “Whatsapp” kuhusu Ukaguzi Maalumu utakaohusisha Maafisa kazi kupita nyumba kwa nyumba na kukagua Mikataba ya Kazi, Mshahara kima cha chini cha Mshahara, Mazingira ya Kazi, malipo ya Hifadhi ya Jamii na fidia kwa Wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa majumbani.
Aidha, tangazo hilo liliainisha faini ya mil 50 kwa kutojisajili kwenye mfumo wa fidia kwa wafanyakazi (WCF). Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa zoezi hilo litaanzia Mkoani Mbeya.
Ofisi inakanusha taarifa hizo na kuueleza UMMA kuwa wapuuze taarifa hizo kwa kuwa hazina ukweli wowote na wala hazijatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambayo ndio yenye dhamana ya kusimamia Sheria za Kazi
Ofisi inawataka watu wanaoeneza taarifa hizo za uongo kuacha upotoshaji huo mara moja. Aidha, Serikali kupitia vyombo mbalimbali inafuatilia taarifa hizi ili kubaini chanzo chake na wahusika, ili kuchukua hatua za Kisheria na haki ionekane inatendeka dhidi yao.
Aidha, Ofisi inatoa wito kwa Waajiri wote kuendelea kutekeleza Sheria za Kazi kwa kuwapatia Wafanyakazi wao mikataba na kuwalipa stahiki zao kwa mujibu wa Sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza katika kaguzi mbalimbali.
Imetolewa na,
KAMISHNA WA KAZI
DODOMA
24/01/2019
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA