Waliobainika Mauaji Ya Watoto Njombe Kuanza Kuburuzwa Mahakamani

Na AMIRI KILAGALILA
Serikali mkoani Njombe inategemea kuanza kuwaburuza mahakamani siku chache zijazo wale wote waliouhusika na mauaji ya watoto wadogo mkoani Njombe kutokana na upelelezi kukamilika kwa baadhi ya kesi

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher olesendeka ameyasema hayo jana mbele ya makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Tanzania bara Philip Mangula katika mkutanao na mabalozi wa halmashauri ya mji mdogo wa makambako pamoja na viongozi wa chama hicho mkoa uliofanyika katika ukumbi wa shule ya secondari makambako mjini humo.

“Tulijipanga vizuri  tuliomba nguvu ya ziada kutoka makao makuu ya jeshi la polisi,tumekwenda vizuri mheshimiwa makamu na wahusika karibu wote tumewapata,tumeamua kuchimba kujua mzizi wa waganga ambao wanaondesha ramli chonganishi na kundi la pili kushughulika na kundi la hawa wanaokodiwa kuondosha uhai wa watu,tumeshugulika na makundi karibia yote tunakwenda vizuri nadhani kuanzia leo na kesho kesi nyingi zitaanza kuunguruma mahakamani kutokana na kukamilika kwa baadhi ya kesi”alisema Olesendeka

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amewatoa hofu wananchi wa mkoa wa Njombe kutokana na taharuki hiyo huku akionyesha kusikitishwa na ushahidi wa awali kuonyesha wahusika wengi wanaohusika na mauaji hayo ni ndugu wa familia hizo.

“Hali ya Taharuki imeondoka tunaenelea na shughuli lakini nikuhakikishie Makamu kwamba hakuna mganga wa jadi aliyehusika katika mauaji haya atakayebaki na hakuna mwananchi aliyehusika na vitendo hivi atakayeachwa bila kufikishwa katika mikono ya sheria,lakini kwa bahati mbaya sana wimbi hili waliohusika ni ndugu wa hawa waliondokewa na watoto wao baadhi yao wanaokamatwa kuhojiwa mpaka sasa ni ndugu wa karibu huwezi kuamini”alisema tena Olesendeka

Naye makamu mwenyekiti wa CCM bara Mzee Philp Mangula amesema kuwa lengo la kukutana na viongozi hao ni kuwakumbusha miongoni mwa malengo ya chama hicho ikiwemo kulinda na kudumisha uhuru wa nchi na Raia wake.

“Nimekuja hapa kuwakumbusheni hilo,tupo katika mazingira ya hofu,wasiwasi na kutiliana mashaka na hofu imetanda hii imetokana na taarifa zisizo za uhakika na uvumi, watu siku hizi mitandaoni wanavumisha mambo hawana uhakika na wanachokisema ni lazima kuondoa taarifa zisizo kuwa na usahihi,taifa zima limeshtuka ndio maana Rais akamtuma waziri wa mambo ya ndani hili jambo ni la hovyo nah ii ni aibu kwa sisi kama wakazi wa mkoa huu na mimi nikiwemo” alisema Mangula

Mpaka sasa jumla ya watuhumiwa 29 wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Njombe kwa ajili ya uchunguzi dhidi ya mauaji ya watoto 7 huku wengi wao wakiwa ni waganga,wafanyabiashara,ndugu pamoja na wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kusababisha vifo vya baadhi ya wananchi waliosadikiwa ni miongoni mwa wauaji wa watoto

Chapisha Maoni

0 Maoni