JE, UNAHISI IPO SIKU KIINGEREZA KITAKUFA, AU KITATAWALA DAIMA?

Swala la lugha katika nchi yetu limekuwa likichukua sura mpya kila leo na swala hili hakika limekuwa ni chachu ya midahalo mingi. Kiingereza, si kwamba ni Tanzania tu, bali pia katika nchi nyingi, kimekuwa ni gumzo. Wapo wadaodaikwamba, kiingereza daima hakiwezi kuanguka kwa kuwa lugha hii imekuwa na mizizi mirefu katika nyanja nyingi za kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na Elimu, utamaduni, michezo, uchumi na teknolojia. Wanaounga mkono hoja hii wamekuwa na mashiko kuwa, kutokana na lugha hii kuendesha nyanja tofauti tofauti katika maendeleo ya watu, basi ndoto ya kusema lugha hii itakuja kufa ni ya alinacha.

Upande wa pili wa sarafu, wapo ambao wanaamini kwamba ipo siku kiingereza kitakufa kutokana na kile kinachoitwa sifa mojawapo ya lugha yoyote ni kufa basi ipo siku hata kiingereza kitakufa. Mara nyingi madai haya yamejikita zaidi kwa mifano ya nchi ambazo zinakuwa juu kimaendeleo-moja ya kitu kinachoilinda lugha yoyote ni hadhi ya maendeleo ya wazungumzaji wa lugha hiyo-na kiteknolojia kama Uchina, Ujapani na zingine nyingi.

Pamoja na madai haya, kumekuwa wanaisimu nguli pia mbalimbali ambao wamefanya tafiti zao za kuhusu matarajio ya kiingereza: kitaendelea kubaki, ama ipo siku kitakufa.

Wanaodai kuwa kiingereza kitabaki kuwa lugha kuu ulimwenguni wameyakita madai yao katika mawazo kuu matatu ya msingi kama ifuatavyo;

  1. Mashiko ya ndani. Katika mashiko ya ndani, wanaodai kuwa kiingereza kitabaki na hadhi yake kwa sababu ya uzuri wake. Kuzungumza kiingereza kwanza kunafurahisha na isitoshe ni kama alama ya utajiri na usomi, katika nchi nyingi.
  2. Mashiko ya nje. Kiingereza kina walimu wengi, nyanja za kufundishia na kujifunzia ni nyingi na pia kina wazungumzaji wengi na hivyo hakitarajiwi kufa.
  3. Mashiko ya matumizi, yaani functional arguements. Katika hoja hii, dai kuu hapa ni kuwa, kiingereza kinatumika katika nyanja nyeti na kubwa katika nchi mbalimbali kama teknolojia, uchumi na elimu, hivyo kutokana na matumizi ya lugha hii, kiingereza kitabaki na hadhi yake ileile ama hata kuendelea mbele zaidi ya kilipo sasa kimaendeleo.
Pamoja na hoja kuu tatu zilizoelezwa hapa juu, zipo pia hoja ndogondogo ambazo zinazidi kushawishi na kuaminisha kuwa, kiingereza kitabaki na hadhi yake. Baadhi ya hoja hizo ndogondogo ni kama ifuatavyo.
  • Matumizi yake kiuchumi. Kazi nyingi zinazofanyika kwa teknolojia zinahitaji na zinatumia lugha ya kiingereza, hivyo kazi hizi kama uhandisi zinaendeleza kukua na kulinda hadhi ya lugha hii-kiingereza.
  • Itikadi. Sehemu nyingi, kiingereza ni alama ya usasa. Kwa hiyo, kuzungumza ama kutumia kiingereza kunamfanya mtu aaminike kuwa anakwenda na wakati.
  • Pia kiingereza kinasimama kama kipimo cha ubora na ufasaha wa mambo anuai yanayoendeshwa katika nchi yoyote ulimwenguni.
Sababu hizi na nyingine nyingi ni ishara ya kuwa, kiingereza bado kinasadikika kuendelea na hadhi yake ambayo kushuka ni vigumu.

Kadri siku zinavyokwenda, zipo pia lugha ambazo zinataka kushika hatamu. Kichina, kwa mfano, ni lugha ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 900, lakini bahati mbaya kilikuwa bado hakijaenea sehemu nyingi ulimwenguni kama kilivyo kiingereza, lakini kwa sasa na kutokana kinvyosambazwa, kinaonekana kuwa tishio la kiingereza. Vyuo vingi sasa vinatoa Elimu ya kichina kwa ngazi ya Shahada ikiwa ni pamoja na chuo kikuu cha Dodoma.

Kiswahili pia ni lugha nyingine ambayo inaibuka kuwa tishio kwa lugha ya kiingereza, kwani kwa tathimini kinatumiwa na watu zaidi ya milioni 120, kikiwa ni lugha ya nne baada ya Kiarabu, kiingereza na kifaransa.

Itaendelea...


Wasiliana moja kwa moja na mwandishi wa Makala hii kwa nambari +255 759 947 397

Chapisha Maoni

0 Maoni