Dar
es Salaam.
Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Eric Shigongo na CCM
wamefikia makubaliano ya malipo ya deni analokidai chama hicho tawala
baada ya awali kuilalamikia sekretarieti kuwa inampuuza.
Shigongo, anayemiliki magazeti na hoteli alilalamika kwenye ukurasa wake
wa facebook na malalamiko hayo kuchapishwa kwenye gazeti moja la kila
wiki kuwa aliingia mkataba wa biashara na CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu
uliopita, lakini chama hicho kimeshindwa kutekeleza wajibu wake na
anapowatafuta wajumbe wa sekretarieti wamekuwa wakimzungusha.
Hata hivyo, Shigongo hakutaja kiasi cha fedha anachoidai CCM wala aina
ya biashara aliyofanya nayo, zaidi ya kueleza kuwa makala hiyo ingekuwa
na mwendelezo.
Lakini jana alifikia makubaliano na CCM. “Nimeitwa na viongozi wa CCM na
tumekubaliana jinsi ya kumaliza tatizo hili,” alisema Shigongo kwa
ufupi alipotafutwa na Mwananchi jana jioni.
Awali jana mchana akizungumza kuhusu malalamiko hayo, msemaji wa CCM,
Christopher Ole Sendeka alisema chama chake hakijapokea barua yoyote
kutoka kwa Shigongo na akamtaka awasilishe nyaraka zake iwapo alifanya
kazi na chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Ole Sendeka alisema utaratibu wa kudaiana uko wazi na anayedai, hupaswa
kukutana na anayemdai na akasisitiza kuwa endapo Shigongo anakidai chama
hicho, awasilishe madai yake sambamba na mikataba aliyoingia badala ya
kulalamika kwenye vyombo vya habari.
“Sitegemei alalamike kwenye mitandao ya kijamii wala kwenye vyombo vyake
vya habari. Kama kweli anatudai, taratibu za kudaiana zipo wazi. Afike
ofisi zetu akiwa na barua yake ya madai, mikataba ya makubaliano ya
kufanya kazi na kiasi cha fedha anazotudai,” alisema.
Katika madai yake, Shigongo alisema juhudi za kumpata Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana ziligonga mwamba, wakati mtu pekee aliyekuwa
akimkuta ofisi ndogo za chama hicho, Zakhia Meghji, ambaye ni mweka
hazina aliyekuwa akimtuliza kwa maneno.
Kinana alipopigiwa simu yake ya mkononi kwa nyakati tofauti, hakupatikana na pia hakujibu ujumbe mfupi wa simu aliotumiwa


0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA