DC Singida: Atakayeugua kipindupindu afikishwe mahakamani

Na Nathaniel Limu, Singida
Watu wawili wakazi wa jimbo la Singida Kaskazini mkoani Singida, wamefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa hatari wa Kipindupindu unaotokana na uchafu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Singida, Elias Tarimo, alisema Novemba, 26 mwaka huu, ugonjwa huo wa Kipundupindu ulibainika katika vijiji vya Merya na Msange jimbo la Singida kaskazini.

Hata hivyo, alisema kuwa ilichukua muda mrefu mno mamlaka zinazohusika kutoa taarifa ya ugonjwa huo, kitendo kilichochangia idadi ya wagonjwa kuongezeka na kufikia 30.

“Urasimu huu umesababisha hatua stahiki za kudhibiti ugonjwa huu, kuchelewa kuchukuliwa na hivyo kuchangia wananchi wawili kupoteza maisha. Kwa sasa tumebakiwa na wagonjwa sita kambi ya Merya na Msange wapo watatu,” alisema Tarimo.

Mkuu huyo wa wilaya, alisema baada ya kupata taarifa hizo kwa kuchelewa, hawakulala walipiga kampeni ya nguvu kuhimiza usafi wa mazingira, matumizi bora ya vyoo na kuchemsha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

“Aidha, wataalam walipima maji ya visima 14 yanayotumiwa na wananchi wa vijiji hivyo, na 12 kubainika vina vidudu vinavyochangia ugonjwa wa kipindu pindu. Baada ya kugundua hivyo, tumepiga marufuku maji ya visima hivyo kutumika,” alisema.

Akifafanua, alisema wamewaelekeza wananchi kutumia maji ya bomba na wamechukua mashine kubwa ya kupampu maji kutoka kijiji cha Sagara.

“Mashine hii tumeisimika na itasambaza maji ya bomba katika vijiji hivyo vya Msange na Merya. Hatujaishia hapo, tunaendelea kuwahimiza wananchi kutumia vidoge vya waterguird kwa ajili ya kutibu maji yawe safi na salama. Vile vile tanawahimiza kutumia vyoo na kuacha tabia ya kujisaidia ovyo kwenye vichaka,” alisema.

Katika hatua nyingine, Tarimo alisema kuwa baada ya kufanya kampeni ya kuhimza usafi, mwananchi yoyote atakayeugua Kipindupindu, atatibiwa na akipona, mara moja atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma ya kutaka kujiuawa kwa makusudi.

Wakati huo huo, katika kuchukua hatua kudhibiti Kipindupindu, Manispaa ya Singida imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo ya kupiga marufuku wafanyabiashara wa matunda, kumenya matunda. Imeagizwa kuwa matunda yote yaliwe nyumbani baada ya kuoshwa vizuri kwa maji.

Pia kila kaya imeagizwa kutumia vyoo bora na kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula chakula na baada ya kutoka chooni.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bravo Kizito Lyapembile, amesema mtu ye yote akikamatwa kwa kuchafua mazingira, atatozwa faini kati ya shilingi 30,000 na 300,000.

Chapisha Maoni

0 Maoni