Mwadui FC sasa yaja kivingine ligi kuu



Tunaweza kusema kuwa timu ya Mwadui FC hivi sasa imekuwa na sura tofauti mara baada ya kupata kocha mpya Ally Bushiri kutoka Zanzibar na kuifanya leo kupata ushindi wa tatu mfululizo katika michuano ya ligi kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo wa leo Mwadui FC imeichapa Kagera Sugar jumla ya mabao 2-1 katika mchezo ulipigwa dimba la Mwadui Complex mkoani Shinyanga na kunyakua point 3 katika mechi ya tatu mfulizo iliyocheza katika dimba hilo.

Mabao ya Mwadui yamefungwa na Awadhi Juma dakika ya 49 na la pili kufungwa na Razak Khalfan dakika ya 85, huku la Kagera Sugar ambao ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao likifungwa na Makalai dakika ya 38.

Kwa ushindi huo Mwadui imezidi kujiimarisha katika msimamo wa ligi kuu kwa kufikisha point 22 na kukwea hadi nafasi ya 8 huku Kagera Sugar ikiwa na point zake 28 katika nafasi ya tano.
Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, Mbeya City imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbao FC na kufikisha point 24 katika nafasi ya 6.

Januari mosi kutakuwa na michezo miwili tu ya kukaribisha Mwaka Mpya ambako Toto African ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na African Lyon ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni