Wahitimu mafunzo ya gesi, mafuta wataka ajira

WANAFUNZI tisa wa Tanzania waliohitimu Shahada ya Uzamili katika masomo ya sekta ya mafuta na gesi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na
Ufundi cha Norway, wameiomba serikali kuacha kuajiri wataalamu wa nje kwa kuwapa nafasi Watanzania waliobobea katika fani hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa na wanafunzi hao waliohitimu masomo kwa udhamini wa Kampuni ya Statoil ya Norway wakati wa sherehe za kupongezwa kwa
kumaliza masomo yao zilizofanyika mwishoni mwa wiki hii Dar es Salaam.
Wahitimu katika masomo hayo ni Nyorobi Kiuga, Idd Mchomvu, Alex Mwang’ande, Adeltus Novat,
Anthony Maswi, Fred Mmkuyi, Kennedy Geoffrey, Shaaban Marco na msichana pekee, Eunuch Jackson.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Eunice alisema kwa sasa Tanzania ina wataalamu wengi katika sekta hiyo waliotokana na ufadhili wa kampuni kadhaa, ikiwamo Statoil ambao wanatoa
fursa ya wanafunzi wa Tanzania kusoma nje kila mwaka.
Alisema hatua ya Kampuni ya Statoil ni ya kupongezwa kwani imelenga kuwapa ujuzi wanafunzi wa Kitanzania ili kuendeleza sekta hiyo kwa kufanya utafiti na masuala mengine na
kuiwezesha nchi kupunguza gharama za kuajiri wataalamu kutoka nje.

Alifafanua kuwa mafunzo waliyopata katika Chuo Kikuu cha Norway ni muhimu sana na kuipongeza
Statoil kwa kudhamini mafunzo hayo na kuwa miongoni mwa wataalamu wa sekta inayokua kwa kasi nchini.
“Changamoto tuliyokuwa nayo ni kuona wapi tutafanya kazi, ajira ni changamoto, sekta hii muhimu sana hapa nchini kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Eunice. Mkuu wa Idara ya Kuongeza Uwezo wa Elimu wa
Kampuni ya Statoil, Profesa Richard Tibaijuka alisema wahitimu hao wamefanya vyema katika masomo hayo kupitia mpango wa mafunzo
ujulikanao kwa jina la Angola-Tanzania Higher Education Initiative (ANTHEI) ambayo hutoa fursa kwa wanafunzi mbalimbali kusoma nje ya nchi
kila mwaka. Profesa Tibaijuka alisema kupitia mpango huo, wanafunzi wa Kitanzania wataendelea kupata
mafunzo hayo kwa kushirikiana na vyuo vikuu mbalimbali katika nyanja tofauti.
Alisema kwa sasa Statoil imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Shule ya Biashara) ili kutekeleza mpango huo na vyuo mbalimbali pamoja na Chuo cha Stavanger cha Norway.

“Mbali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwepo kwenye mpango huo, pia Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimejumuishwa katika mpango huo
ambapo chuo hicho (Udom) watashirikiana na Chuo Kikuu cha Barcelona kutoa Shahada ya
Uzamili wa fani hiyo kwa msaada wa maabara iliyotolewa na Statoil,” alieleza Profesa Tibaijuka.
“Statoil inajivunia kufanya kazi na vyuo
mbalimbali katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi, lengo letu ni kuona sekta hii inapata maendeleo makubwa sana. Mpaka sasa jumla ya wahandisi 32 wamepatikana katika mpango huu
ambao ulianza mwaka 2012 na utamalizika mwaka 2019,” alifafanua.

Chapisha Maoni

0 Maoni