Serikali yatangaza neema kwa watumishi wa umma



WALIMU na watumishi wengine wenye sifa watapandishwa madaraja katika mwaka wa fedha 2017/18, baada ya uhakiki wa watumishi kukamilika, Bunge liliambiwa jana mjini hapa.



Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum  (CCM), Mary Mwanjelwa.

Mbunge huyo alitaka kujua mkakati na sera ya serikali kwa wafanyakazi hususan walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara.

Jafo alisema kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, watumishi hupandishwa vyeo kwa kuzingatia sifa na ufanisi katika utendaji kazi.

"Mwalimu anapohitimu mafunzo yake anastahili kubadilishiwa muundo wake wa utumishi. Mfano, mwalimu daraja III stashahada kwenye daraja II ngazi ya Shahada,"alisema.

“Kupanda daraja kwa mtumishi kunategemea utendaji kazi utakaothibitishwa na matokeo katika Mfumo wa Wazi wa Upimaji utendaji Kazi (Opras) kwa mtumishi husika.

Alisema watumishi wote wanatakiwa kujaza fomu hizo na kupimwa utendaji wao kama wanastahili kupandishwa madaraja.

Aidha, alisema kama ilivyoelezwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, walimu, wakiwamo watumishi wengine wenye sifa watapandishwa madaraja katika mwaka wa fedha 2017/18 baada ya kukamilika uhakiki wa watumishi.

Chapisha Maoni

0 Maoni