Mbwana Samatta katika ubora wake


Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Ally Samatta amerejea kwenye ubora wake baada ya jana kucheza kwa dakika 68 na kuisaidia timu yake ya KRC Genk kuibuka na ushindi wa 1-0 ugenini.

Samatta ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitatu jana amecheza mchezo wake wa tatu tangu apone majeraha ya mishipa ya paja ambayo aliyapata Novemba 4 mwaka jana.

Genk jana imeshinda mchezo wake wa Ligi kuu nchini Ubelgiji dhidi ya wenyeji Royal Excel Mouscron kwenye uwanja Le Canonnier mjini Mouscron, Ubelgiji.

Baada ya Samatta kutoka nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji kutoka DR Congo, Dieumerci N'Dongala ambaye alifunga bao pekee la ushindi katika mchezo huo dakika ya 83.

Jumanne wiki hii Samatta aliichezea Genk na kutoa pasi ya bao la kwanza la timu yake lakini bao hilo halikusaidia timu hiyo kushinda kwani ilifungwa 3-2 ugenini dhidi ya Kortrijk katika mechi ya Kombe la Ubelgiji.

Chapisha Maoni

0 Maoni