SAKATA LA WAFANYA KAZI HEWA LAZIDI KUCHUKUA SURA MPYA, MFANYA KAZI ALIYEKO MASOMONI JAPAN ACHUNGUZWA.

SUALA la kusaka watumishi hewa limeendelea kushika kasi nchini baada ya mikoa kadhaa kutangaza kuikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) kuchunguza kwa kina huku watendaji waliohusika wakisimamishwa kazi.

Mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa huo, Said Mecky Sadiki, ameagiza kusimamishwa kazi Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, William Msapali na kutaka Takukuru imchunguze mtumishi Agapit Chuwa aliyepo masomoni nchini Japan kwa miaka 13.

Sadiki, ameagiza Halmashauri ya wilaya ya Mwanga kumsimamisha kazi Msapali kwa madai ya kushindwa kutoa ushirikiano wakati wilaya hiyo ikihakiki watumishi hewa na kuwabaini 21 ambao wameisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 199. Alisema tuhuma nyingine kwa Msapali ni kushindwa kubainisha taratibu zilizomruhusu mtumishi wa sekta ya afya, Chuwa ambaye mwaka 2004 aliomba kibali kwenda masomoni nchini Urusi ambapo alijiongezea muda na sasa yupo nchini Japan huku akilipwa mshahara.

Sadiki aliitaka Takukuru pia kumchunguza mtumishi huyo aliyepo masomoni kwa zaidi ya miaka 13 kwani ameisababishia serikali hasara ya Sh milioni 54. Kutokana hilo, Sadiki alitaka taratibu kufanyika ili kusitisha mshahara kwa mtumishi huyo na kuitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na baadaye kumfikisha mahakamani mtumishi huyo aliyepo masomoni na wengine wote walioisababishia serikali hasara.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jamhuri William alisema hakuna kumbukumbu za kutosha za taarifa za Chuwa ingawa alipewa ruhusa ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2004.

Alisema mtumishi huyo alikuwa akijiongezea ruhusa kwa kushirikiana na maofisa Utumishi waliokuwapo ingawa baadaye tena alipewa ruhusa nyingine mwaka 2014 hadi 2016 kuendelea na masomo katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema barua ya kuomba ruhusa ya mtumishi huyo iliandikwa lugha ya Kijapan lakini pia kwa Kiingereza ambacho hakikuwa kinasomeka vizuri jambo lililosababisha badala ya kupewa ruhusa ya miaka miwili, akapewa ya miaka mitatu.

Awali katika taarifa yake kwa mkuu huyo wa mkoa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaibu Ndemanga alisema wilaya hiyo yenye jumla ya watumishi 2,048 ilitambua watumishi hewa 21 walioisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 199.

Alisema walitumia hati ya malipo ya Septemba mwaka jana na kwenda katika kila ofisi kujua kama wahusika wapo ofisini ambapo 17 walikuwa wagonjwa, 14 waliomba ruhusa, 20 walikuwa likizo, 26 watoro, 26 walihama lakini bado walisomeka kwenye hati ya malipo

Chapisha Maoni

0 Maoni