MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Seleman Manoti, kifungo cha miaka
miwili jela kwa kupatikana na hatia ya kujifanya usalama wa Taifa.Hata
hivyo, mahakama imetoa hukumu hiyo bila mshitakiwa kuwepo mahakamani
kutokana na kuruka dhamana kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa.Akitoa
hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema kuwa upande wa
mashitaka, ulileta mashahidi wanne kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma
hizo.
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhishwa na
ushahidi huo na kwamba mahakama inamtia hatiani mshitakiwa licha ya yeye
kutokuwepo.“Hati ya kumkamata mshitakiwa itolewe na adhabu hii itaanza
kutumika pindi mshitakiwa atakapokamatwa kwani alitoroka akiwa na haki
ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Haule.Wakili wa Serikali, Ester Kyara
aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa
wengine.Inadaiwa kuwa Novemba 19, 2014 maeneo ya Kariakoo Msimbazi
wilayani Ilala, mshitakiwa alijitambulisha kwa Issaya Odelo na Charles
Odinga kuwa Ofisa Usalama wa Taifa, kitu ambacho alijua si kweli. Katika
hatua nyingine, kondakta Ally Salum (23), mkazi wa Mwananyamala,
amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia
ya kuiba daladala.Mbali na mshitakiwa huyo, Exavery Kaunga (44) ambaye
ni mlinzi na mkazi wa Kiwalani, Minazi Mirefu, aliachiwa baada ya
ushahidi dhidi yake kuwa na shaka.Akitoa hukumu hiyo jana katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan,
alisema kuwa upande wa mashitaka ulileta mashahidi wanne kuthibitisha
kosa hilo.“Nimeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka,
nakutia hatiani mshitakiwa kama ulivyoshitakiwa kwa kutumikia kifungo
cha miaka mitano jela,” alisema Hakimu Hassan.Kabla ya kutolewa adhabu
hiyo, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba mahakama kutoa adhabu
kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine. Hata hivyo, mshitakiwa
alipoulizwa ni kwa nini asipewe adhabu kali, hakujibu chochote na
mahakama kutoa adhabu hiyo.
Washitakiwa hao walishitakiwa kwa makosa
mawili ya kula njama kutenda kosa ambapo inadaiwa kati ya Julai 5, mwaka
jana, washitakiwa walikula njama kutenda kosa.Pia inadaiwa Julai 5,2015
pembezoni mwa barabara ya Nyerere katika Kituo cha Mafuta cha Victoria,
washitakiwa waliiba gari lenye namba za usajili T 624 CSH aina ya
Eicher mali ya Kampuni ya White Swan.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA