WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
kusimamia Menejimenti ya Mamlaka hiyo katika Idara ya Utawala na
Rasilimali Watu kuhakikisha ajira zote zinazotolewa zinazingatia sifa na
vigezo vya kuajiri.
Akizungumza katika uzinduzi wa Bodi hiyo mpya jijini Dar es Salaam jana
pamoja na mambo mengine, Profesa Mbarawa aliisisitiza bodi hiyo
kuifanyia kazi Ripoti ya Uchunguzi wa uendeshaji wa viwanja hivyo nchini
na kufanya mabadiliko mara moja.
“Nataka muipitie ripoti niliyomkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mkuu na mfanyie
maamuzi, suala la kuajiri watu kiholela, ninataka wote walioandikwa
kwenye ripoti hiyo kuwa hawana sifa watolewe wapishe watu wenye sifa ili
waweze kufanya kazi”, alisema.
Aidha, Profesa Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kusimamia kwa uadilifu
miundombinu yote ya viwanja vya ndege nchini na kuhakikisha mashine za
ukaguzi zinafanya kazi saa 24 ili kudhibiti mianya yote ya rushwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Ninatubu Lema
alimhakikishia Waziri huyo kuwa ataongeza ushirikiano na wafanyakazi
wote na kusimamia maagizo yote yaliyotolewa.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA