Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, ameahidi kuacha kutumia lugha ya
matusi baada ya kile anachosema kuwa ni kupata ujumbe wa moja kwa moja
kutoka kwa Mungu.
Rais huyo, alliyemwita Rais Barack Obama "mwana wa kahaba" na akasema
kiongozi huyo anaweza "kwenda jehanamu", amesema amefikia uamuzi huo
baada ya kupata ufunuo alipokuwa safarini kutoka Japan.
Amewatusi pia watu wengine mashuhuri. Alimwita kiongozi wa kanisa
Katoliki duniani Papa Francis "mwana wa kahaba" (Ufilipino ni taifa
lenye Wakatoliki wengi).
Amewahi kumtusi pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kwa
kumuita "mwendawazimu" na majuzi alimweleza balozi wa Marekani nchini
Ufilipino kama "mpenzi wa jinsia moja ambaye ni mwana wa kahaba".
Bw Duterte amesema kuwa alipokuwa kwenye ndege, na watu wengine wote
walikuwa wamelala, alisikia sauti ikimuonya: usipokoma, nitaiangusha
ndege hii.
Amesema sauti hiyo ilijitambulisha kuwa ilitoka kwa Mungu.
Amewaahidi watu waliokusanyika mji wake wa nyumbani wa Davao kwamba ahadi kwa Mungu ni sawa na ahadi kwa Wafilipino.
Rais Duterte ni kiongozi ambaye msimamo wake na matamshi yake huzua utata mara kwa mara.
Amesomea taaluma ya sheria na alipanda cheo hadi kuwa mwendesha mashtaka
kabla ya kuteuliwa kuwa naibu meya wa Davao wakati wa mapinduzi
yaliyomuondoa madarakani Ferdinand Marcos mwaka 1986.
Alikuwa meya mwaka 1988 na kushikilia wadhfa huo kwa kipindi cha miaka
10, kabla ya kushinda kiti cha ubunge katika Bunge la Congress halafu
akarejea kwenye kiti cha umeya mwaka 2001.
Alijijengea umaarufu kwa kupiga vita baadhi ya matatizo makubwa
yanayowakabili Wafilipino - uhalifu, makundi ya uasi, na ufisadi. Yote
haya yalipungua kwa kiwango kikubwa wakati alipokuwa kiongozi wa Davao,
na kufanya mji huo kuwa mmoja wa miji salama zaidi nchini Ufilipino.
Duterte ambaye utawala wake ni wa kipekee kwa kuwa kiongozi mwenye sera
za Kijamaa na mwanamageuzi kwa pamoja, sera zake za uchumi zilikuwa si
za kuaminika wakati wa kapeni.
Majuzi, alilinganisha vita vyake dhidi ya walanguzi wa mihadarati na mauaji ya Wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Alisema anaweza kuua walanguzi wengi wa dawa hizo za kulevya sawa na alivyofanya Hitler akiua Wayahudi.
"Hitler aliua Wayahudi milioni tatu ... kuna waraibu milioni tatu wa dawa za kulevya. Ninaweza kufurahia sana kuwaua," amesema.
Wayahudi zaidi ya milioni sita waliuawa na Wanazi chini ya Hitler..
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA