Mradi wa kuweka mashine za utambuzi wa vidole katika jeshi hilo ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ya Bunge, Naghenjwa
Kaboyoka jana alithibitisha taarifa hiyo ya utekelezaji kukabidhiwa kwa
Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali
Projest Rwegasira.
Alisema Katibu Mkuu huyo alifika kwenye kamati ya PAC jana na kutoa
taarifa kuhusu kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya
Bunge.
“Baada ya taarifa hiyo kupelekwa Ofisi ya Bunge, Spika Job Ndugai
akishaipokea ndiyo ataiwasilisha kwa kamati ya PAC,” alisema Kaboyoka.
Alibainisha baada ya Katibu Mkuu wa Wizara kutoa taarifa kwa kamati juu
ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge, PAC
haikujajadili tena taarifa hiyo.
Lugumi ilikuwa inatekeleza mradi wenye thamani ya Sh. bilioni 37 wa
kusimika mfumo wa utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi
nchi nzima.
Mwanzoni mwa Aprili, PAC ilieleza kuwa kampuni ya Lugumi ililipwa Sh.
bilioni 34 na Jeshi la Polisi mwaka 2011 ili kufunga vifaa hivyo katika
vituo 138 vya polisi nchini, lakini ni vituo 14 tu ndivyo vilivyokuwa
vimefungiwa, licha ya kulipwa fedha hizo ambazo ni sawa na asilimia 90
ya malipo yote ya kazi hiyo.
Ulipaji wa asilimia 90 ya malipo ya kandarasi kabla ya kukamilika kwa kazi ni kinyume na sheria ya manunuzi ya umma.
Wakati wa kuahirishwa kwa kikao cha bajeti Juni 30, Naibu Spika, Dk.
Tulia Ackson alisema Bunge limeagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo
unafanya kazi, na pia Kamati ya PAC ifuatilie na kutoa taarifa katika
taarifa ya mwaka ya kamati.
Alisema kamati ilibaini kuwa mradi huo unafanya kazi katika vituo 14
pekee kati ya 108 jambo ambalo lilikuwa linaenda kinyume na mkataba.
Aidha, Dk. Tulia alisema kutokana na changamoto hiyo kamati ya PAC
ilimtaarifa Spika, ambapo aliwaruhusu kuunda kamati ndogo ambayo nayo
ilifanya ukaguzi na kubaini mapungufu.
Naibu Spika alisema baada ya kamati hiyo kuipitia, ilikubaliana
kukabidhi taarifa hiyo kwa Spika ambapo na yeye ameona kuwa inastahili
kuwasilishwa.
Alisema kwa mujibu wa kanuni Spika ataweka utaratibu wa kujadili taarifa
ya kamati endapo kamati yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake
itaona kuwa kuna mambo ya utekelezaji inaweza kutoa taarifa maalum kwa
waziri husika ili aweze kuchukua hatua zinazostahili.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA