Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha na mkazi wa kata ya Sakina,
Alistalius Silayo (45) amefikishwa mahakamani akituhumiwa kumnajisi
mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 11.
Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Pennina Joackim
ilidai kuwa mfanyabiashara huyo alitenda kosa hilo katika vipindi
tofauti kati ya Januari na Septemba mwaka huu.
Mwendesha Mashitaka alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya
ya Arusha, Patricia Kisinda kuwa mshtakiwa alikuwa akifanya kosa hilo
mara kwa mara katika miezi hiyo eneo la Sakina kwa Iddy yaliko makazi
yake.
Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 158 Kifungu
kidogo cha 1(a) cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na kufanyiwa
marekebisho 2002.
Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana shitaka hilo na hakimu
alisema dhamana iko wazi ya wadhamini wawili wanaotambulika kisheria.
Mbali ya hilo, pia wadhamini hao lazima wawe na mali isiyohamishika
yenye thamani ya zaidi Sh milioni 10 na wadhamini hawaruhusiwi kutoka
nje ya Mkoa wa Arusha bila ya kibali cha Mahakama.
Hata hivyo, wadhamini hao walishindwa kukamilisha taratibu za dhamana
mahakamani hapo na hakimu aliwapa muda kukamilisha taratibu katika saa
za kazi na kuamuru mshtakiwa kurudishwa rumande hadi taratibu
zitakapokamilika.
Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 10, mwaka huu kwani Mwanasheria wa Serikali alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA