KITENDO cha serikali kumpa notisi ya siku 90 ya kumfutia umiliki wa
shamba la ekari 33 Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu kimemfanya
mwanasiasa huyo kujitokeza na kusema hatikiswi na kitendo hicho,
anaandika Charles William.
Taarifa ya William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi iliyotolewa jana, ilisema Sumaye amepewa notisi ya siku 90 kabla
ya kufutiwa umiliki wa shamba hilo lilipo eneo la Mabwepande jijini Dar
es Salaam.
“Kama ulifikiri wewe ni Waziri Mkuu mstaafu kwahiyo tutashindwa
kukuchukulia hatua, tumechukua hatua na hatuangalii sura ya mtu,”
alisema Lukuvi.
Akitolea ufafanuzi wa suala hilo, Sumaye amesema, “Kwanza bado sijapewa barua yoyote, ni hila za kisiasa tu.
Wakati Paul Makonda akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC) nilienda naye pale akawambia wananchi waondoke.
“Lakini nashangaa DC wa sasa (Ally Salum Hapi) alienda pale kuwambia
wananchi hao wasiondoke kwasababu Rais John Magufuli anataka kulifuta
lile shamba.
Nilienda mahakamani na ikaamuriwa kusiwe na shughuli yoyote, nasubiri tarehe ya kesi ambayo mwanasheria wangu ndiyo anaijua.”
Sumaye ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), amesema tangu alipojiunga na upinzani mwaka jana
amekuwa akiandamwa kwa mambo yanayoshangaza.
“Nina shamba kule Mvomero, Morogoro nililolipata kwa kufuata taratibu
zote. Ndani ya shamba hilo kuna nyumba ya kuishi, ng’ombe zaidi ya 200,
mbuzi 300 lakini nikepewa notisi ya kulifuta kwa kuwa sijaliendeleza.
Nimeenda mahakamani pia ambako ndipo mahali pekee ambapo haki itapatikana.
Kama walidhani kwa kunifanyia hivi nitarudi Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wasahau, hata kama nilikuwa na nia hiyo sirudi.” Amesema Sumaye.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA