YA ZITTO NA NAPE, ANGALIA HAPA WALIVYOJIBIZANA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII


ZITTO AACHE UNAFIKI

Na Nape Nnauye (MB)

NAZIONA juhudi kubwa za Mbunge wa Kigoma Mjini Ndg. Zitto Kabwe kujaribu kupotosha jamii kwa kutosema ukweli kuhusu masuala kadhaa yahusianayo na Muswada wa Huduma za Habari, 2016.

Kwa kawaida mimi huwa sio mtu wa kujibu hoja zinazotolewa kinafiki na kioga kama
alivyofanya rafikiangu Zitto Zuberi Kabwe. Kwa hali ya kawaida ningeweza kumpuuza kabisa, lakini kwa hili uvumilivu wangu kwa kiwango hichi cha unafiki umefikia ukingoni. Hivyo nitalazimika kujibu baadhi ya hoja.

Nimesoma kwa masikitiko sana sana, makala ndefu kidogo aliyoisambaza ndugu yangu na mwanasiasa kijana mwenzangu Ndg. Zitto Zuberi Kabwe kuhusiana na alichodai ni hatari ya Mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari 2016.

Muswada huu uliochapishwa na kuwekwa hadharani tangu Septemba, 2016, pamoja na mambo mengine unakwenda kuhitimisha safari ya zaidi ya miaka 20 ya wadau wa habari nchini kuwa si tu na sheria nzuri itakayoratibu kazi na kulinda maslahi yao, bali sheria inayoitangaza rasmi kazi hii kuwa taaluma kamili.

Hata hivyo, akiyatumikia maslahi yasiyo wazi kwa sasa, akiongozwa na unafiki wa hali ya juu kabisa kupata kuushuhudia kwake, na baada ya kujaribu kuzuia muswada huu kwenye Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na juhudi zake hizo kushindwa vibaya. Mbunge mwenzangu Zitto Kabwe ameanza kupayuka mitandaoni akieneza uzushi na kila aina ya uongo na upotoshaji kuhusu muswada huu.

Inahitaji ujasiri wa kinafiki kuandika aliyoyaandika mwanasiasa mwenzangu kijana Zitto Zuberi Kabwe. Licha ya kuwa nimekuwa nikimheshimu kwa muda mrefu, na bado namheshimu na kumpenda kama kijana mwenzangu, unafiki huu wa kutumikia masilahi binafsi umenistua sana.

Kama nilivyosema nitayajibu baadhi ya madai yake kama ifuatavyo:-

#1. Hoja ya Kushirikishwa wadau:
Zitto anajaribu kujenga picha kuwa muswada huu haukushirikisha wadau. Ndugu yangu huyu, huku akiwa anajua kuwa katika utungaji wa mswaada kuna hatua mbili za kutoa maoni.

Hatua ya kwanza ni pale ambapo serikali inapokuwa inatengeneza mswaada husika kabla ya kuupeleka kwenye vikao vya kiserikali kwa hatua za kuupitisha wadau HUSHIRIKISHWA ili kutoa maoni yao. Na kwa mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari ,2016 WADAU wameshirikishwa tena na ushahidi wa maandishi wa ushiriki wao na maoni yao UPO.

Hatua ya pili ya utoaji maoni huwa ni baada ya mswaada kusomwa mara ya KWANZA bungeni, Mswaada husika hukabidhiwa kwa Kamati husika ya Bunge, na ukishakabidhiwa huwa ni waraka huru kwa umma kuusoma na kutoa maoni yao( public document) kwa Kamati ya Bunge.

Hili pia limefanyika mpaka hatua ya wadau kuitwa na kuja Dodoma ambapo waliomba mbele ya Kamati wapewe muda wakamilishe kazi ya kusoma na kutoa maoni yao. Na Mwenyekiti wa Kamati Ndg. Peter Serukamba(mb) kwa uamuzi wa Kamati ya kudumu ya Bunge wakaamua kuwaongezea muda wadau kwa wiki moja kukamilisha kazi hiyo, shughuli inayoendelea sasa.

Ndg. Zitto kwa makusudi aliamua kujaribu kuzuia hatua hii ya pili isifanyike bila mafaniko.
Hoja yake hiyo ilianguka mbele ya Kamati tulipoonesha ushahidi wa wazi na wa nyaraka kuwa wadau wakuu wote si tu walishiriki katika hatua za ndani ya Serikali kutoa maoni na sasa watashiriki zaidi katika hatua hizi za Bunge bali sehemu kubwa ya maoni yao yaliingizwa katika muswada wa sasa. Zaidi ya asilimia 90+% ya maoni ya wadau yamezingatiwa katika Mswaada huu.

Alipoona kashindwa kabisa akaamua kuondoka Dodoma akasafiri na kusambaza waraka wa kizushi ili kufurahisha waliomtuma badala ya kuchangia kuboresha mswaada husika.

#2. Hoja ya kulazimisha vyombo vya Habari nchini kujiunga na TBC:-
Zitto pia anaeneza uongo kwamba muswada huu unadhamiria kuvifanya vyombo vya habari hususani TV kulazimishwa kujiunga na TBC kwenye vipindi vyake.

Kwanza nina wasiwasi kama ameusoma muswada huu na kama ameusoma naanza kuamini hana muswada sahihi. Au ndio kaamua kutoa maoni akiongozwa na unafiki.

Hata hivyo hili tumelifafanua katika Kamati, kwa bahati mbaya hakuhudhuria ili kupata uelewa mpana. Mosi hakuna kifungu kama hicho katika muswada huu; pili, hakuna dhamira hiyo kwenye muswada huu; na tatu, serikali haina hata wazo hilo.

#3. Mitandao ya kijamii:
Zitto katika kutimiza malengo na maslahi yake, anapotosha kuwa muswada huu unakusudia kuzibana blogs na kutaja mitandao ya kijamii kama JamiiForums kuwa nayo itatakiwa kusajiliwa.

Mtu huyu ni wa kumwonea huruma. Bahati mbaya muswada huo hauna mamlaka wala nia hiyo. Kifungu cha 3 cha Sheria kiko wazi kuwa usajili utahusu magazeti na majarida na machapisho yao ya mitandaoni(magazeti mtandao ya magazeti hayo rasmi na sio mitandao yote au mingine ya kijamii kama anavyopotosha).

Na kwakuwa nakala ya Mswaada huu ina tafsiri ya kiingereza na Kiswahili sitaki kuamini kuwa Zitto hakusoma hili, au waliomtuma hawakusoma vizuri hili.

Zitto anakwenda mbali kudai wachangiaji kama wa jamiiforums watatakiwa wafanyiwe ithibati! Bila shaka mwenzetu huyu anajadili muswada mwingine kabisa.

Muswada huu hauhusu wala hakujapata kuwa na fikra za kudhibiti au kuratibu mitandao ya kijamii na kuwataka watumiaji wa mitandao hiyo eti wasajiliwe. Huu ni upuuzi mwingine wa kupuuzwa.

#4. Ipo hoja ya Waziri kupewa mamlaka kuagiza chombo chochote kutangaza jambo lenye umuhimu kwa umma:
Katika hili pia tumsamehe kwa sababu hahudhurii vikao vya Kamati wakati wa mijadala hii. Hili limejadiliwa kwa kina na wahusika kuelewana. Hakuna kifungu kinachompa mamlaka hayo Waziri.

Bali kifungu kilichopo kinaipa fursa Serikali kuvishauri/kuvielekeza(Govt MAY) vyombo vya habari kuungana pamoja kulinda maslahi ya Taifa kunapokuwa na jambo la muhimu kama vile nchi kuwa VITANI au majanga makubwa. Zitto kama kijana wa Kitanzania kama haoni umuhimu wa hili basi hakuna namna nyingine ya kumsaidia.

#4. Kwamba muswada unampa Waziri wa Habari majukumu ya kutoa masharti kwa kazi za vyombo vya habari na kwamba anaweza kuamua gazeti lichapishwe habari aitakayo:
Hili ni eneo lingine linalothibitisha kuwa hapa tunajihusisha na mtu mwenye malengo ya hatari sana na anayejaribu kuweka matazamio yake katika jambo la muhimu kama hili.

Muswada huu hauna kifungu hicho zaidi ya Waziri kupewa uwezo wa kisheria, kama ilivyo katika sheria nyingine, kutunga kanuni za kutekeleza sheria hii. Hili nalo Zitto hataki!

#5. Zitto anasema muswada huu unampa mamlaka Waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe nchini:

Ni kweli muswada umetoa mamlaka hayo lakini Zitto ameamua kutosema ukweli wote.

Muswada unampa Waziri mamlaka hayo si kwa kila jarida au kitabu bali yale tu ambayo yamedhihirika kuchapisha habari huku yakivunja sheria za nchi. Kama Zitto anafikiri nchi yetu itaruhusu majarida yanayotaka kuhamamsisha vita na uvunjifu wa amani nchini, ajue hakuna nchi inayoruhusu mambo hayo.

#6. Zitto anazungumzia kuwepo kwa vifungu vya uchochezi akitoa tafsiri kuwa wabunge wa upinzani watabanwa:
Kwanza katika hili lazima ijulikane kuwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Kimataifa Juu ya Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966, masuala yote yanayohusu kusababisha athari kwa usalama wa taifa ni ukomo unaokubalika wa uhuru wa habari (allowable restriction to press freedom).

Uandishi wa habari kama taaluma nyingine unabeba haki na wajibu. Moja ya masuala ambayo waandishi wanapaswa kubeba wajibu kwayo ni kutosababisha hatari kwa usalama wa Taifa kwa kusababisha vurugu, chuki katika jamii(uchochezi). Hivyo katika kuweka vifungu hivi muswada umezingatia ukweli huo wa sheria za kimataifa.

Hata hivyo ieleweke, tofauti na Zitto anavyopotosha, sheria hii imekwenda mbali zaidi kwa ruhusu wananchi na watu wengine kuikosoa Serikali na utekelezaji wa sera zake.

Sheria inasema haitakuwa uchochezi kama mtu atatoa maoni yake kwa minajili ya kukosoa makosa katika Serikali, makosa katika utekelezaji wa sera (kifungu cha 49[2]). Huu ni uhuru mkubwa sana kuwahi kutamkwa na sheria.

Mwisho, namshauri Ndugu Zitto Kabwe apunguze kuishi kinafiki. Akasome tena muswada huu na alete hoja zake kwenye Kamati ya Bungeni zijadiliwe, aache kupotosha umma mitandaoni na aache kujiweka karibu zaidi na vibaraka.

Muswada huu, narudia tena, unakwenda kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma inayoheshimika. Ni muswada unaokwenda kuipa heshima taaluma hii na kila mmoja wetu awe tayari kwa mageuzi haya.

Katika kuifanya fani hii kuwa taaluma tunafahamu kuwa wapo waliozoea mambo ya kale na yale yale na kwamba watapinga; tunafahamu wapo watakaoona wanahabari waliowaajiri watadai maslahi zaidi na wapo watakaoona fani hii kuwa taaluma kamili watashindwa kuitumia kwa maslahi yao- wanahabari na wananchi tuungane kuwakataa wenye maslahi binafsi katika hili.

Tuungane kutoa maoni ili tuwe na muswada bora zaidi na utakaoifanya sekta ya habari kuwa na mchango mzuri zaidi kwa nchi yetu.

Kwasasa niishie hapa, lakini nitaendelea na awamu ya pili hata ya tatu ya ufafanuzi ikibidi. Uzalendo katika hili utashinda unafiki na utumwa wa kubeba mawazo ya watwana wachache walizoea vya kunyonga ambavyo kuchinja kwao msamiati!


----------------------------------
Majibu ya Zitto Kabwe kwa Nape Nnauye
----------------------------------

Majibu yangu Kwa HOJA za Nape Nnauye kuhusu muswada wa Huduma za habari, 2016

Ndugu yangu Nape Nnauye amejibu andiko langu nililolitoa Jana kuhusu muswada tajwa. Kama ilivyo ada ya Siasa za kijinga jinga Nape amejibu andiko langu Kwa kunishambulia binafsi na kuweka Hoja zake mbalimbali. Mimi sitamjibu Nape namna yake maana wenye busara wametufunza ' when they go low go high '.

Nitajibu Hoja za Nape Na sitamjibu Nape. Hata kwenye andiko langu sikutamka neno Nape Nnauye kwani Siasa zangu sio Siasa za mtu bali za masuala. Sitahangaika Na mtu bali Hoja ili kujenga.

1. Hoja ya Kushirikishwa wadau
Nape anasema:

Majibu ya Hoja hii:

Kanuni za Bunge(kanuni ya 84 ) zinataka kwamba Muswada ukishasomwa Kwa mara ya kwanza Bunge lifanye MATANGAZO Kwa umma ili kuhakikisha kuwa umma unaelewa maudhui ya muswada na kuwezesha Wananchi kutoa maoni Yao. Muswada huu kwanza Bunge halikutoa matangazo yeyote (Kwa Taarifa tu Ni kwamba Hata Kamati ya Bunge ilishindwa kutoa photocopy nakala za uchambuzi wa muswada kutoka Kwa wanasheria wa Bunge Kwa sababu Bunge halina Fedha.

Bunge halina Fedha kutoa photocopy ya nyaraka za Wabunge kufanyia Kazi ). Wadau wote waliokuja mbele ya Kamati ya Bunge walitamka dhahiri kwamba wamepewa Taarifa ya kutokea mbele ya Kamati Siku 2 kabla ya vikao Na hivyo wameomba muda zaidi wa kutoa maoni Yao. Labda Ni kutokana Na uchanga wa shughuli za Bunge, Waziri anajenga Hoja kwamba Ushiriki ulianzia kabla.

Mtu yeyote anayejua namna Bunge linavyofanya Kazi atakwambia muswada Ni muswada pale ambapo umechapishwa kwenye gazeti la Serikali Na kusomwa mara ya kwanza Bungeni. Wadau wote waliiambia Kamati kwamba Kwa muswada huu Ndio walikuwa wanashirikishwa Kwa mara ya kwanza pale mbele ya Kamati.

Hivyo wadau hawakushirikishwa kwenye muswada huu tangu umesomwa Kwa Mara ya kwanza Bungeni. Kama Serikali ina ushahidi wowote ule kwamba kati ya Septemba Na sasa muswada huu umehusisha mdau yeyote waweke wazi uthibitisho huo. Nyaraka zinazoonyeshwa Na Serikali Ni za miaka ya nyuma kabla ya muswada kuwa muswada. Ushirikishaji unaanza rasmi pale muswada upo gazetted Na umesomwa Bungeni.

2. Hoja ya kulazimisha vyombo vya Habari nchini kujiunga na TBC
Nape anasema:


Majibu ya Hoja:

Itakumbukwa kuwa muswada wa awali ulikuwa Na kifungu hiki Na wadau wakapiga kelele sana kukataa. Ukisoma muswada huu Kwa juu juu utaweza kuona kuwa kifungu hiki hakipo. Mtu mwenye dhamira ovu huficha huficha mambo yake. Kwenye muswada huu mambo mengi yaliyokataliwa Na wadau sasa yamewekwa kiujanja Kwa kuweka Mamlaka hayo Kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari.

Serikali inaposea hakuna kifungu hicho haisemi kuna kifungu gani. Nitawaeleza kifungu kilichowekwa ambacho ndicho kitatumika na Waziri kufanya haya bila kuhojiwa Na mtu yeyote yule, kupitia kanuni.

Sehemu ya 7(1)(b)(iv) inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari Fulani au masuala Fulani yenye umuhimu kwa Taifa.

Serikali itatumia kifungu hiki kutekeleza jambo lile lile ambalo wadau walikataa kuwekwa sheria Siku za nyuma. Serikali italiweka Kwa mlango wa nyuma. Mbaya zaidi muswada unatamka wazi kwamba Waziri mwenye dhamana ataweka TERMS and CONDITIONS Kwa uendeshaji wa 'media houses'. Hivyo Hata wakifuta kifungu Hicho cha 7, bado Waziri kapewa Mamlaka makubwa sana ya kuamua Chombo cha habari kinaendeshwaji.

Ni dhahiri kwamba Waziri ama anajua haya au kawekewa vifungu ambavyo yeye binafsi hajui tafsiri zake lakini atashangazwa katika utekelezaji wa sheria. Kifungu cha 60(2)(a) ( Minister to make regulations for TERMS and CONDITIONS for OPERATIONS of licensed media house) inampa Mamlaka hayo Waziri kiasi ambacho ataweza kuendesha vyombo vya habari atakavyo yeye. Muswada huu unamfanya Waziri wa Habari kuwa Mhariri Mkuu wa Taifa.

3. Mitandao ya kijamii:


Majibu ya Hoja:

Muswada uliopo mbele ya kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana sana ya vyombo vya habari. Sehemu ya 3 ya Muswada inatamka chombo cha habari ni pamoja na gazeti, kituo cha radio na televisheni ikiwemo mitandao ya kijamii (online platforms).

Napenda umma wa Watanzania ufahamu kwamba muswada Ni wa Kiingereza. Muswada wa Kiswahili Ni Kwa ajili tu ya kuwezesha Wabunge wasiojua kiingereza kuweza kuelewa vifungu vya muswada. Muswada Ni wa Kiingereza, Ndio rasmi. Mahakamani hawatatumia muswada wa Kiswahili Bali muswada rasmi.

Tafsiri ya online platforms haikuwekwa kwenye muswada. Tafsiri ya media Ndio imeweka Hilo la online platforms. Naomba mtu yeyote aende Google Na kuandika online platform atapata tafsiri ni Nini. Nitsaidia kidogo hapa.

Social media is defined as “online interactions among people in which they create, share, and exchange information and ideas in virtual communities, networks and their associated platform”.

Serikali itatumia tafsiri hii ya kwenye muswada kubana mitandao ya kijamii. Hivi Watanzania mmesahau kesi ambazo Wananchi wanapewa kupitia sheria ya cyber crime? Hivi mnasahau kuwa Rais alisema anatamani mitandao ya kijamii Malaika washuke waizime? Malaika watashuka Kwa kupitia muswada huu. Muswada huu una nia ovu kabisa ya kukandamiza uhuru wa habari.

Pia...


Majibu:

Msomaji utaona dhahiri kuwa hakuna Hoja ya kujibu hapo. Hivi CNN inaagizwa kisheria Na Serikali ya Marekani kuhusu kulinda Nchi Yao? Hivi hapa Tanzania kuna Chombo cha habari binafsi ambacho kinaweza kwenda kinyume Na Nchi wakati wa vita? Muswada umetaja vita? Maelezo ya Waziri yanaonyesha dhahiri kuwa Serikali haina Hoja bali inahangaika kuokoteza Hoja. Kwenye hili Sina la kujibu majibu yamo ndani ya maelezo Yao.

4. Kwamba muswada unampa Waziri wa Habari majukumu ya kutoa masharti kwa kazi za vyombo vya habari na kwamba anaweza kuamua gazeti lichapishwe habari aitakayo.

Majibu:

Nimeeleza huko juu kuhusu Mamlaka haya ya Waziri wa Habari. Kifungu cha 60 kipo wazi sana.

5. ...muswada huu unampa mamlaka Waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe nchini:

Majibu:

Nadhani wenye uelewa wanaelewa maana ya hili. Sina maelezo ya kujibu hili kwani linajitosheleza.

Nani anatafsiri maslahi ya umma?
Nani atafsiri kuwa sheria za Nchi zimevunjwa Kama sio mahakama?
Kwanini kabla ya Waziri kufungia vitabu au magazeti asipate amri ya mahakama?
Yeye Waziri Ni Nani Mpaka atoe tafsiri ya kitabu Fulani au gazeti Fulani limevunja sheria?

6. Kuhusu kuwepo kwa vifungu vya uchochezi akitoa tafsiri kuwa wabunge wa upinzani watabanwa:

Majibu:

Sina maelezo katika hili. Wenye uelewa wanaelewa namna Hoja za namna hii hutumika.

Kiufupi masuala yote ya uchochezi yaliyokuwa kwenye sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 yamerudishwa kwenye sheria hii mpya.

Sheria hii inakwenda mbali Na kusema "Hata ukitamka jambo ambalo linaweza kujenga chuki ya Wananchi dhidi ya Serikali Ni uchochezi".

Mwisho:


Napenda kutoa ushauri wa bure Kwa ndg. Nape Nnauye, kwamba kujadiliana Kwa Hoja kuna Maslahi Kwa Nchi.

Wote waliosoma andiko langu wataweza kutofautisha vijembe, dharau, kulewa madaraka Na matusi kwenye majibu ya Nape Na Hoja kwenye andiko langu. Katika andiko langu sikumtaja Nape Kwa jina Kwa sababu najua anatimiza wajibu wake Kama Waziri.

Katika majibu yake kuanzia mwanzo Mpaka mwisho Ni vijembe tu. Hii inaonyesha uwezo wetu mdogo wa kuhimili mijadala. Hii Ndio inayofanya Watanzania tuonekane watu ambao hatukusoma au tulikwenda shule lakini hatukuelimika.

Haiwezekani kwamba mtu yeyote ambaye ana Hoja tofauti Na wewe atakuwa ametumwa. Kwamba hatuna uhuru wa mawazo binafsi Na hivyo lazima tutumwe. Hii Ni hulka mbaya sana ambao sikutegemea Kama wanasiasa vijana wanaweza kuiendeleza. Lakini Kama kuna mtu ambaye amezoea kutumwa Hoja Ni dhahiri kwamba anaona mwengine yeyote mwenye Hoja nyengine katumwa Pia.

Ninaamini muswada huu Ni mbaya Na unadidimiza uhuru wa habari. Ninaamini kuwa muswada huu Kama ulivyo haupaswi kujadiliwa Na Bunge Kwa sababu unapaswa kuandikwa upya.

Muswada huu ukipitishwa hakuna mchapishaji(printer) wa magazeti atakayekubali kuchapisha magazeti sababu Kwa mujibu wa muswada Mkurugenzi wa Maelezo anaweza kuingia kwenye mtambo wowote akiwa Na Polisi Na kuung'oa. Haya sio kwamba hayajaanza kufanyika, yamefanyika.

Wakati wa masuala ya UKUTA kuna wachapishaji walikataa kuchapisha gazeti lolote lililokuwa na neno UKUTA. Watu wa magazeti wanajua hili Na wanaweza kuthibitisha Kwa namna wanayoona inafaa.

Mimi nimeandika. Nimetahadharisha. Nimetimiza wajibu wangu.

Chapisha Maoni

0 Maoni