NINI KIFANYIKE ILI ELIMU YETU IWE YENYE HADHI? USHAURI WANGU KATIKA UBORESHAJI WAKE.


Elimu, kama wengi wetu tunavyoamini, ndiyo msingi, ama ufunguo wa maisha na maendeleo katika ujumla wake. Labda kwa kifupi, katika falsafa, hasa wanafalsafa Mwl Nyerere na John Dewey wanaamini kwamba, huwezi kutenganisha Elimu na Maendeleo kwa namna yoyote ile. Nasema hivyo kwa sababu, wapo wengi wanaoamini kuwa, mtu anaweza akaendelea hata bila elimu; na katika hili, wamekuwa na mifano ya watu kadha wa kadha ambao wanadaiwa kuwa na maendeleo ya hali ya juu kuliko hata ya wenye elimu. Lakini katika hili niseme tu kwamba, wanasahamu nadharia kuu ya elimu kuwa
, si tu kwa kupata mafunzo rasmi darasani ndiyo kuwa na elimu, Elimu ni neno pana asana. Kwa kufupi, elimu haiishii tu kuwa na cheti, lakini uhalisia sahihi ni ujuzi sahihi unaobakia kichwani ambao aidha umepatikana kwa kuhudhuria darasani, ama hata katika mtaala mwingine Zaidi.
Katika ufafanuzi wangu, ningependa kutumia falsafa ya elimu (Educational philosophy) ambayo bila shaka inakidhi mahitaji ya uchambuzi wa Makala hii juu ya nini kifanyike ili kuihuisha hadhi ya elimu yetu.

Falsafa ya elimu ni njia muhimu ya kukabiliana na changamoto za elimu kabla ya kuzitolea ufafanuzi. Kwa kawaida, Falsafa ya elimu hupatikana kwenye kitu kinachoitwa Mitaala, na kwa bahati nzuri sana, Tanzania tunayo mitaala mizuri na bora kabisa ambayo nitaizungumzia kwa  ufupi sana katika Makala hii.
Mtaala wa elimu ya msingi.
Katika ukurasa wake wa kwanza kabisa, mtaala huu unachambua mahitaji muhimu ya kiuchumi, kijamii na kwa mtu mmoja mmoja. Lakini eneo muhimu hapa nitakalo kuligusia ni changamoto za utoaji elimu inayokidhi mahitaji bainishwa. Moja ya kitu kinachotajwa katika mtaala huu ni upatikanaji rasilimali watu; kwa kuanza na Mwalimu mkuu anayetajwa katika mtaala huu ni mwenye sifa hizi;
·         Awe amehitimu kidato cha nne na ufaulu angalau daraja la tatu na kuendelea,
·         Awe amepitia chuo na kuhitimu ngazi ya stashahada na kuendelea,
·         Awe na uzoefu usiopungua miaka mitano
Pamoja na hayo, mtaala unataja pia mwalimu na uhusiano wake na wanafunzi ambapo mwalimu mmoja anatakiwa kufundisha wanafunzi 40 (1:40). Vipindi pia kwa wiki moja vinatakiwa kuwa kati ya 28 na 32 kwa kila mwalimu. Wakaguzi pia ni rasilimali watu nyeti inayotakiwa kuwepo kwa kipindi kinachohitajika.
Sanjari na hayo, rasilimali vitu pia ni eneo muhimu ambalo limebainishwa kwenye mtaala huu ambalo linajumuisha vitu muhimu kama;
·         Vitabu vya kiada na ziada vitakavyokuwa vimepitishwa na kamati ya wizara yenye dhamana chini ya udhibiti wa vifaa wa elimu, mfano tunacho chombo muhimu sana cha udhibiti wa vifaa vya elimu, Educational Materials Approval Committee (EMAC)
·         Samani na majenogo ikiwa ni pamoja na maktaba zenye kiwango cha hali ya juu sana.
Nimeanza na elimu ya msingi ambayo naamini ndiyo msingi wa madaraja mengine ya elimu, na katika mambo yaliyotajwa katika mtaala wake, kuna vitu ambavyo vimekuwa vikipuuzwa na kuchukuliwa, kama si muhimu, vya kawaida sana.
Nianze na rasilimali watu. Kwanza kwa sifa za mwalimu mkuu ambaye mtaala inamtambua nia suala ambalo limekuwa kikwazo, kwani ni wachache wenye kiwango kilichogtajwa hapa. Ufaulu mara nyingi umekuwa ni ule wa kiwango cha daraja la nne ambao haukumuwezesha kuendelea na masomo ya elimu endelevu. Lakini pia, wengi wao hawana stashahada ya elimu kama inavyobainishwa, wengi wao wana kiwango cha ngazi ya cheti.
Uhusiano wa mwalimu na wanafunzi pia ni Zaidi ya mtaala unavyobainisha, kwani shule nyingi za msingi zina mafuriko ya wanafunzi ambao wanazidi idadi stahiki iliyobainishwa katika mtaala huu.

Tatizo linguine ni rasilimali vitu, tatizo ambalo limekuwa sugu kwa muda mrefu sasa. Shule nyingi hazina majengo na maktaba. Nitoe tu mfano kwamba, shule niliyowahi kusoma ilikuwa na maktaba ambayo pia ni ofisi ya mwalimu mkuu. Mbali na kuwa ofisi, vitabu vyake pia havina uhusiano na masomo yanayofundishwa, mfano ilikuwa imejaa sana vitabu vya riwaya za kiingereza ambazo mtoto wa shule ya msingi hawezi hata kuzisoma, na vingine vya jiographia za nchi zingine.

Kando na hilo, vitabu pia vinavyozalishwa havimpi uwezo mtoto wa kufikiria. Mfano hai kwa sasa, vitabu vya maswali na majibu vya kina NYAMBARI NYANGWINE ambavyo vimejaa karibu masomo yote kama JIPIME KATIKA HISABATI, SAYANSI, KISWAHILI n.k. Kinachofanyika hapa ni kumuwezesha mtoto kuwa na uwezo mkubwa wa kukariri, na si kuelewa.
Tatizo linguine lililojitokeza hivi karibuni ni kubadirisha mfumo wa mitihani. Mfano, mtihani wa HISABATI ambao zamani tulikuwa tukifanya kwa SWALI, KAZI, JIBU, lakini leo hii unakuja na majibu ya kuchagua; kitu ambacho kinatoa elimu ya kubahatisha.
Vyumba vya madarasa havikidhi mahitaji ya mtaala. Nilikuwa siamini kama kwa karne hii kungekuwepo na shule ambazo watoto wanasoma chini ya mti, lakini nilipotembelea shule ya msingi Nyahua, iliyopo Sikonge, ndilo nilipoikuta hii hali na kunifanya nipigwe na butwaa. Karne ya 21 bado mtoto anasoma kama mtumwa! Kwa hili, serikali isilifumbie macho kabisa.
Ukaguzi pia umekuwa duni sana. Katika awamu hii, kuna malalamiko ambayo yanadaiwa kuwa, serikali imefuta posho kwa wakaguzi wa shule. Niseme tu kwamba, kwa kufanya hivyo, ni kutengeneza mwanya wa kuua kabisa elimu, kwani shule kujiendesha yenyewe ni sawa na kichaa kumkabidhi rungu!
Masuala haya yaangaliwe kwa jicho la tatu, na kwa kufanya hivyo, naamini elimu itapata hadhi ambayo itakidhi mahitaji muhimu ya jamii.


Chapisha Maoni

1 Maoni

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA