Imefichuka..Hii Hapa Sababu ya Nyuma ya Pazia ya Uteuzi wa Mhe Mghwira Kuwa RC Kilimanjaro


MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mgwira, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kile kilichoelezwa kuwa ni “mkosoaji mwenye faida” na kwamba Rais John Magufuli bado ana nafasi kwa wote wanaomkosoa kwa hoja na si vinginevyo.

Hatua hiyo inatajwa kumweka Magufuli katika taswira ya kukanganya zaidi kwa kuwa tayari amepata kutoa kauli zinazokandamiza siasa za upinzani nchini, ikizingatia kuwa Juni, mwaka jana, alitangaza kusitisha mikutano ya kisiasa akitoa ruksa kwa wabunge pekee hali iliyozua malumbano kati yake na viongozi wa vyama vya upinzani.

Vile vile akiwa Zanzibar, katika mikutano ya hadhara, mwaka jana, alimshangaa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na wapinzani ambao anaamini hawakustahili kuwamo kwenye serikali hiyo.

Lakini kwa sasa Raia Mwema limeambiwa na mmoja wa wandani ya Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam kwamba uteuzi huo si wa mwisho na kwamba Rais Magufuli haamini kwamba kuna watu wameumbwa kuwa wapinzani maisha yao wote.

Hii ni mara ya kwanza kwa mmoja wa wandani wa Rais Magufuli kueleza kinagaubaga kuhusu uteuzi huo wa Mghwira ambaye alikuwa mshindani wa mgombea huyo wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Nenda kawaambie Watanzania kwamba Mghwira amechaguliwa kwa sababu ya constructive criticism (ukosoaji wenye hoja) yake. Rais hana shida na wakosoaji wa namna hiyo na siku zote wana nafasi kwa serikali yake.

“Hata Profesa Kitila Mkumbo naye alikuwa anamkosoa Rais Magufuli mara kwa mara lakini bado alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Hii ni kwa sababu siku zote Kitila alikuwa akimkosoa kwa haki na kwa hoja.

“Sasa kuna wakosoaji wengine kila siku wanakosoa tu na wakati mwingine wanaweka matusi na kashfa humohumo. Watu kama hawa Rais Magufuli hawezi kufanya nao kazi.

“Na naomba wewe mwenyewe nikupe home work ya kujiuliza nini maana ya mwanasiasa wa upinzani. Je, maana yake ni kupinga kila kinachofanywa na serikali iliyo madarakani?

“Kwa tafsiri ya Rais Magufuli, hakuna mpinzani wa kudumu. Yeye anaamini vyama visivyo madarakani ni vyama mbadala tu kwa CCM na haimaanishi kazi yao ni kupinga tu bila hoja. Ujumbe kwa wanasiasa wote ni kwamba yeye hana ubaguzi na yuko tayari kufanya kazi na wote wenye hoja, Raia Mwema limeambiwa na chanzo chake hicho cha uhakika kutoka Ikulu.

Polepole azungumza

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisisitiza kwamba rais amefanya uteuzi huo kwa kuzingatia kigezi kikuu cha Utanzania wa mteuliwa.

“Ni rais wa Watanzania wote anapofanya uamuzi huzingatia katiba na sheria za nchi. Amepewa mamlaka kikatiba kuteua wasaidizi wake wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya, msingi wa kwanza katika uteuzi ni Utanzania wa watu hao anaowateua na mengine kama uadilifu.

Hizi ni zama za CCM mpya tunatazama uadilifu na kuzingatia watu wenye fikra na mwelekeo sawa na ule wa rais wetu, kuendeleza mapambano ya kuelekea uchumi wa kati ambao kimsingi ndio uchumi wa viwanda.

Rais anapofanya uamuzi hafungwi, kuna maeneo anaelekezwa na kuna maeneo anaachwa afanye kutokana na imani ya wananchi juu yake. Rais anapoteua Watanzania wanaweza kutoka popote kwenye vyama vya siasa au hata vyombo vya ulinzi, kuna askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania amewateua kuwa wakuu wa wilaya kwenye wilaya za pembezoni mwa nchi, hawa bado ni askari walioko kwenye utumishi wa jeshi,” alisema Polepole.

Chapisha Maoni

0 Maoni