BAADHI ya wanachama wa ACT-Wazalendo wilayani Mbarali, wanatajwa kusuka
njama za kuhujumu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutengeneza tuhuma dhidi
ya mbunge wa jimbo hilo Haroon Mulla na kuzisambaza mitandaoni.
Taarifa
zinamtaja Dk. Anthony Mwandulami aliyekuwa meneja wa kampeni wa mgombea
ubunge wa jimbo hilo kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Dickson Kilufi kuwa
ndiye anayesuka mipango hiyo ili kumchafua kisiasa mbunge huyo. Kwa
mujibu wa mawasiliano yaliyonaswa, Dk.Mwandulami ambaye pia ni
mfanyabiashara na mganga wa kienyeji, amekuwa na mawasiliano ya mara kwa
mara na Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na ujangiri Robert Mande na
inaelezwa ni kumpa taarifa za mbunge huyo, ambapo mawasiliano ya
karibuni ni 24, Oktoba majira ya saa 1:06 jioni, ambapo walizungumza kwa
dakika 281. Taarifa zaidi zinasema, wakati huo ambao Mwandulami
akiwasiliana na Mande, askari wa kikosi cha kupambana na ujangili
walikuwa kwenye shamba la uwekezaji la mbunge huyo wakichimba kile
kinachodaiwa ni kutafuta meno ya tembo yanayaodaiwa kufukiwa shambani
hapo. Inaelezwa askari hao hawakufanikiwa kukuta meno ya tembo na badala
yake kwenye upekuzi wao walikuta nyama ya swala ambayo ilihifadhiwa
baada ya wahusika kuwinda kwa kutumia kibali walichonacho.
Hata hivyo,
askari hao walichukua nyama hiyo na kudai ni nyara ya serikali ambapo
baadaye mtoto wa mbunge huyo anayeitwa Fahad Pirmohamed, anayesimamia
shamba hilo alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20
jela au kulipa faini ya Milioni 138 ambayo walilipa na kuachiwa huru.
“Kuna jambo lipo nyuma ya kesi hii na kilichopo ni siasa tena za
kuchafuana, Dk.Mwandulami alimpigia kampeni Kilufi, wakashindwa na
wameenda kukata rufaa mahakamani dhidi ya Haroon Mulla, wakati kesi
inaendelea, kunaibuka madai ya mbunge kuhusika na meno ya tembo na
kinachotia mashaka zaidi siku moja kabla ya kesi ya kupinga ubunge
kuanza kusikilizwa, usiku zinasambazwa taarifa kwamba mbunge anahusishwa
na ujangiri na kweli kwake kulipekuliwa” alisema mtoa taarifa ambaye ni
mkazi wa Mbarali. Aidha, mwananchi huyo ambaye hakutaka jina lake
litajwe alisema anachofanya Dk. Mwandulami ni kucheza siasa za majitaka
ili kuhakikisha heshima ya mbunge huyo inashuka na ikibidi kumuondolea
uhalali wa kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo ili kumpa nafasi Kilufi
aliyeshindwa akiwa CCM, akahamia Chadema ambako alikosa nafasi ya
kuteuliwa kugombea ubunge na kuhamia ACT aliposhindwa ubunge. “Mchezo
mbaya zaidi anaofanya Dk. Mwandulami ni kupeleka taarifa za uongo hata
kwa waziri Maghembe (Waziri wa Maliasili na Utalii) na hata ukiangalia
kuna mawasiliano walifanya Oktoba 23 saa nne usiku na walizungumza kwa
dakika 19, sasa Waziri naye amedanganywa, TANAPA nao wameingizwa mkenge
na kutumika kwenye mchezo huu wa kisiasa” alisema mtoa taarifa huyo.
Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa, tayari baadhi ya vyombo vya habari
likiwemo gazeti la Mtanzania ambalo liliripoti habari hiyo, wamebaini
mchezo huo wa kisiasa na tayari wamemuomba radhi mbunge Haroon Mulla
huku taarifa za ndani kwenye Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
wakisita kutoa ufafanuzi wa suala hilo baada ya kubaini vita za kisiasa
kwenye suala hilo. “Hadi leo TANAPA wapo kimya, walisema watatoa taarifa
juu ya suala hilo lakini wanasita maana wamegundua kuna siasa
zinachezwa na kuna upotoshwaji unafanywa na mtu ambaye ana malengo yake
binafsi, nashauri viongozi wetu wawe makini maana kuna upotoshwaji
mkubwa unaendelea kwenye suala hili”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA