Mtu
mmoja anayesadikiwa kuwa ni jambazi alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na
askari Polisi kisha kufariki dunia wakati akipelekwa katika hospitali ya
Monduli kwaajili ya matibabu.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Naibu Kamishna Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea usiku maeneo
ya Makuyuni barabara ya Arusha-Makuyuni wilayani Monduli.
“Mara baada ya kulisimamisha gari hilo wakaanza kumpora abiria mmojawapo
aliyejulikana kwa jina la Victor Pius (46) Mfanyabiashara, mkazi wa
Majengo Moshi ambapo walichukua simu mbili aina ya Nokia na Samsung
pamoja na fedha taslimu Tsh 50,000/=,” Alisema Kamanda Mkumbo.
“Wakati wanaendelea na tukio hilo askari Polisi waliokuwa high way
patrol walipata taarifa za tukio hilo ambapo walikwenda kwa haraka na
mara baada ya majambazi hao kuwaona walianza kufyatua risasi hovyo na
polisi kuanza kujibu mapigo na kufanikiwa kumjeruhi mmoja wao na
kuwakamata wengine kumi na mbili papo hapo wakiwa na mapanga sita na
marungu manne huku wengine akiwemo na yule mwenye bunduki wakikimbia,”
aliongeza.
Aidha Kamanda Mkumbo alisema jambazi huyo akiwa na wenzake wapatao 29
walikuwa na bunduki ambayo bado haijafahamika pamoja na silaha za jadi
mapanga na marungu ambapo waliweka mawe barabarani na kulisimamisha gari
aina ya Fusso lenye namba za usajili T. 871 BUZ ambalo lilikuwa lina
mzigo likitokea Moshi kuelekea mkoani Singida.
Kamanda Mkumbo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huu kuendelea
kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu ili
zifanyiwe kazi kwa haraka, huku akitoa onyo kwa majambazi wanaopenda
kujipatia kipato bila kuvuja jasho kwani Jeshi hilo limejiandaa vizuri.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA