Napenda kuchukua fursa hii kwa heshima kubwa kabisa na kwa niaba ya
wananchi wenzangu wa Jimbo la Nzenga Mjini kumpongeza Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa
uamuzi aliouchukua wa kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na kumfuta kazi mwenyekiti wa Bodi hiyo‘
‘Bw. Bernard Mchomvu, kwa kutofuata maagizo ya Mhe. Rais na matakwa
ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 31 na 32
ambavyo vinaelekeza Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali kuweka
fedha zao katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu.’
‘Uamuzi huo sio tu unawanufaisha walipa kodi wa Taifa letu lakini pia
unakomesha tabia za matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma kwa
kujitajirisha na kujinufaisha isivyo halali kwa baadhi ya Watendaji
Wakuu wa Mashirika ya Umma‘
‘Pamoja na kuwa Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Kikwete alisaini Sheria
namba 5 ya Benki Kuu tarehe 7 Juni 2006 miaka takribani kumi iliyopita
hakuthubutu kuchukua uamuzi mgumu na wenye manufaa kwa Taifa kama
uliochukuliwa na Rais Magufuli wa kuamua kuweka fedha za mashirika ya
Umma katika Akaunti Maalumu zilizopo Benki Kuu‘
‘Kutokana na uamuzi huu wa Rais Magufuli, zaidi ya Shilingi bilioni
564.6 za ikiwa ni jumla aya shilingi na fedha za kigeni katika akaunti
267 za Mashirika ya Umma na Idara za Serikali zimeokolewa zisiingie
katika mikono ya ‘wapiga dili’ ambao walizoea kutumia mwanya huo
kujinufaisha isivyo halali kwa fedha za walipa kodi wa Taifa letu‘
‘Katika hatua za kuendelea kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli,
ninamshauri achukue hatua zaidi ya zile alizozichukua kwa iliyokuwa Bodi
ya TRA, kwa kuwa mtindo wa kuweka fedha za umma katika mabenki ya
biashara una harufu ya ufisadi, wizi wa fedha za umma na dalili za
matumizi mabaya ya madaraka ndani ya miaka 10 iliyopita‘
‘Ni vema Mhe. Rais ikimpendeza akafikiria kuanzisha uchunguzi maalumu
(forensic audit) kubaini kupitia mwanya huo wa kuweka fedha za umma
kwenye benki za biashara Je Serikali ilipoteza fedha kiasi gani kwa njia
ya dili chafu, na kubaini endapo kulikuwa na matumizi mabaya ya
madaraka, kufunua mwanya wa kuondoa hisia na viashiria vya ufisadi, wizi
na rushwa katika hatua za kuwekwa fedha hizo katika akaunti za fixed
deposits‘
‘Hatua hii italisaidia Taifa kuwafikisha mbele ya mkono wa Sheria
maharamia wote na wapiga dili walioliingiza Taifa letu katika hasara
kubwa kwa manufaa yao wenyewe. Ikiwezekana hatua dhidi yao zichukuliwe
kwa mujibu wa Sheria za uhujumu uchumi ili mahakama ya Mafisadi
iliyoundwa na Mhe. Rais Magufuli ifanye kazi yake kwa kasi‘
‘Aidha, katika hatua nyingine ili kuziba kabisa mianya ya upotevu wa
fedha za umma katika hatua za kudumu, ninamshauri Mhe. Rais Magufuli
katika Bunge lijalo mapema mwaka 2017 apeleke Bungeni kwa hati ya
dharura, marekebisho ya Sheria Namba 5 ya Benki Kuu ya mwaka 2006 ili
kurekebisha vifungu vya 31 na 32 na vifungu vyake vidogo‘
‘Katika uchambuzi wangu wa Sheria hii nimebaini ipo mianya ya
kisheria ambayo inaweka ulaini katika masharti ya kulazimisha Mashirika
ya Umma na Idara za Serikali na Serikali za Mitaa kuweka ulinzi wa fedha
za umma kwa kuzitunza katika akaunti zilizopo Benki kuu na badala yake
kufungua dirisha la kuziweka fedha hizo katika benki za biashara kwa
mujibu wa sheria‘
‘Kwa mfano, kifungu cha 32 cha Sheria Na. 5 ya BoT ya mwaka 2006
kinasema kuwa, ninanukuu “32.–(1) The Bank, in its capacity as a banker
and fiscal agent of the Governments or of any public authority, may be
the official depository of the Governments or public authority concerned
and accept deposits and effect payments for the account of the
Governments or public authority.” Katika taaluma ya Sheria, neno “may be”
‘Linamaanisha sio lazima kwa mujibu wa sheria kuweka fedha za
Mashirika ya Umma na idara za Serikali katika akaunti za BoT. Huu ndio
ulaini wa sheria ninauzungumzia ambao ulitumiwa miaka 10 iliyopita
kuweka fedha za umma katika akaunti za Benki za Biashara. Ili kuweka
msingi mzuri wa uamuzi wa Mhe. Rais Magufuli ni vema kifungu hiki
kikabadilishwa ili kulazimisha Mashirika ya Umma kutunza fedha zao BoT
kwa mujibu wa Sheria‘
‘Pia kwa kuwa juhudi za Mhe. Rais Magufuli zimeongeza ukasanyaji wa
mapato kwa kodi, ninamshauri kwa kuwa sasa Serikali inaondoa zaidi ya
Shilingi 1 trilion kwa mwezi kutoka kwenye mifuko ya Watanzania kwa njia
ya tozo za kodi na wakati huo huo kupitia sheria tumeondoa fedha za
mashirika ya Umma kutoka kwenye Mabenki ya Biashara kuna Umuhimu wa
Serekali kuhakikisha Fedha zilizotengwa kwenda kwenye Miradi ya
Maendeleo zinakwenda kwa kasi ili kuchochea mzunguko wa fedha kwenye
Uchumi. Hatua hii itasaidia sana ku-stimulate uchumi na kupunguza
mdororo unaoanza kujitokeza‘
‘Aidha pia, Namshauri Mhe. Rais kufanya marekebisho makubwa katika
mfumo mzima wa uanzishaji, uendeshaji na uratibu wa biashara nchini ili
kuongeza ajira nchini, kwa kuwa ripoti ya Benki ya Dunia (2016) ya
kufanya biashara Tanzania (Doing Business Tanzania- 2016)‘
‘Inaonesha Tanzania kutofanya vizuri katika Sera na Sheria za usajili
wa biashara mpya na mazingira ya uendeshaji wa biashara kuwa kushika
nafasi ya 129 kati ya nchi 189. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mjasiriamali
akitaka kuanza biashara rasmi lazima avuke vihunzi 9 ndani ya takribani
siku 26 ili aweze kufungua biashara yake! Vihunzi hivyo vinavunja moyo
na kupunguza kasi ya ongezeko la ajira binafsi kwa njia ya ujasiriamali
na pia inalipa Taifa hasara kwa kutokusanya kodi kutoka kwenye biashara
hizi mpya kwa haraka na kwa wakati kutokana na urasimu uliopo‘
‘Pamoja na hayo pia, namshauri Mhe. Rais, agize wizara ya wiwanda na
biashara na wizara ya fedha kurekebisha sheria za kodi na biashara ili
kuwezesha wepesi, urahisi na uharaka wa kukusanya kodi na kuwezesha
wafanyabiashara wadogo kufanya biashara kwa uhuru‘
‘Ripoti ya Doing Business Tanzania, (2016) imebainisha kuwa makampuni
yanayolipa kodi huchukua saa 179 kujaza fomu za marejesho hivyo
kuifanya Tanzania kuwa na utaratibu mgumu wa kulipa kodi na kushika
nafasi ya 150 kati ya nchi 189 duniani kwa ugumu wa taratibu za kulipa
kodi. Tukiondoa ugumu huo na kuweka wepesi, kasi ya kukusanya mapato ya
kodi itaongezeka na mapato pia yataongezeka!‘
‘Kwa umahususi Serikali inaweza kuanzisha kituo kimoja cha biashara
kwa wafanyabiashara wadogo (one stop business center) kitakachotoa
motisha kwa kuratibu uanzishaji wa biashara husika mpaka kulipa kodi kwa
njia za digitali na mifumo ya TEHAMA. Vituo hivi viwepo kuanzia ngazi
ya Serikali za Mitaa ili kurahisisha shughuli za uanzishaji wa Biashara
na uwekezaji kutokea chini‘
‘Marekebisho hayo ya sheria za kodi na biashara yalenge zaidi
kutengeneza ‘Business Incubation’ na Misamaha ya kodi (Tax holidays) kwa
wafanyabiashara wadogo wanaoanza biashara ili kusaidia kukuza biashara
kuliko hali ilivyo hivi sasa ambapo biashara ndogo zinakabiliwa na mzigo
mkubwa wa kodi na Tozo za ushuru mbalimbali katika halmashauri zetu kwa
mfano Leseni, kodi ya huduma, kodi ya mapato, na kodi za majengo‘
‘Pia kama taifa umewadia wakati Mhe. Rais awaagize BoT na Wizara ya
Fedha katika kipindi cha miaka hii mitano ya awali kubadili ‘Modeli ya
Uchumi’ wetu kutoka ‘Consumption module’ kwenda kwenye ‘Investment
module’ na hii iendane na mabadiliko makubwa ya ‘Tax structure’ yetu na
sheria za Uwekezaji na Biashara na kutengeneza motisha (Incentive
package) za kisekta na si motisha za ya mwekezaji mmoja mmoja‘
‘Sekta muhimu ambazo zinahitaji kupewa kipaumbele kwenye hiyo new module ni sekta ya ngozi, na viwanda vya mazao ya kilimo‘
‘Mwisho kabisa napenda kumhakikisha Mhe. Rais kuwa mimi binafsi kama
mbunge, wananchi wa Jimbo la Nzega na Watanzania wengine wote tunaoamini
katika uadilifu katika ofisi za umma, tunaendelea kumuombea ulinzi kwa
Mungu, na tupo nyuma yake kumuunga mkono dhidi ya vita hii ngumu ya
kupambana na ‘wapiga dili’ walioligeuza Taifa letu miaka 10 iliyopita
kuwa shamba la bibi‘
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA