Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 03 Novemba, 2016 amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika
nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na
kuzungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania yenye
thamani ya jumla ya Dola za Marekani Bilioni 1.6 zikiwa ni mkopo kutoka
benki hiyo.
Akizungumza baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi.
Bella Bird amesema mikopo hiyo inalenga kusaidia juhudi za maendeleo
nchini Tanzania na itatolewa katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati,
usafirishaji, elimu na maji.
"Miradi hii yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo
katika maisha ya Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na
msukumo mzuri kutoka Serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni
kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia maendeleo" amesema Bi.
Bella Bird.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea
kushirikiana na Tanzania katika maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo
kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi.
"Tunataka kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi
kuzungumza, miradi hii ina manufaa makubwa kwa watanzania na tungependa
utekelezaji wake ufanyike haraka, na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia
inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa" amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya
Awamu ya Tano imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote
inayotekelezwa sasa na itakayoanza kutekelezwa katika siku zijazo kwa
mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kwa hivi sasa miradi 26 yenye thamani ya Jumla ya Dola za Marekani
Bilioni 4.5 inatekelezwa hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Novemba, 2016
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA