Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa amri ya
kukamatwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kuamuru wadhamini
wake kufika mahakamani hapo kujieleza kwanini wasilipe fungu la dhamana
kutokana na mshtakiwa huyo kushindwa kufika kusikiliza kesi yake bila
ruhusa.
Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio.
Amri hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya
upande wa Jamhuri kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa jana kutajwa lakini
mshtakiwa wa nne Lissu hakuwepo mahakamani.
Hata hivyo, alijitokeza mdhamini wake mmoja kati ya wawili Robart Katula
kudai kuwa mshtakiwa huyo anaendesha kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu
Tanzania, Kanda ya Mwanza.
Hakimu alihoji kwa nini mshtakiwa amesafiri na kuacha kuhudhuria kesi yake bila kuomba kibali cha mahakama yake.
"Mshtakiwa Lissu anafanya dharau kila wakati inapopangwa kesi yake
mahakamani anashindwa kuhudhuria bila kutoa sababu ama kuomba ruhusa ya
mahakama... kama asingekuwa nje kwa dhamana angefanyaje? angetumia
busara kuomba ruhusa" alihoji na kuongeza kuwa.
"Wadhamini wa mshtakiwa wapelekewe wito wa mahakama waje kujieleza
kwanini wasilipe fungu la dhamana kama walivyoahidi kwenye hati ya
dhamana ya maneno ya Sh. milioni 10 kila mmoja" alisema Hakimu Simba.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Patrick Mwita aliomba mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa mshtakiwa.
Hakimu Simba alikubali ombi la Jamhuri na kutoa amri ya kukamatwa
mshtakiwa na wito kwa wadhamini kufika mahakamani Novemba 21, mwaka huu
kujieleza kwa nini wasilipe fungu la dhamana dhidi ya mshtakiwa kwa
kushindwa kuhudhuria kesi yake.
Mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni, Wahariri wa gazeti la Mawio,
Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka
huu, Dar es Salaam, Lisu na wenzake walikula njama ya kuchapisha
chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari
kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia Lissu na wenzake walidaiwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam,
kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali
ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye
uchochezi.
Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka
waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia
kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA