Mwanaume mkazi wa Ilala, Siwema Seif (40) amehukumiwa na Mahakama ya
Mwanzo ya Ilala kwenda jela mwaka mmoja kwa kumtolea lugha ya matusi na
kumdhalilisha kimwili, Zainab Ramadhan ambaye ni mama yake mzazi.
Akisoma hukumu mahakamani hapo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Matrona
Luanda alisema ushahidi uliotolewa na shahidi namba moja ambaye ni
mlalamikaji, ulionesha kukosa shaka na kumtia hatiani mshitakiwa.
Shahidi huyo alisema siku ya tukio mshitakiwa alifika nyumbani kwao
akaomba chakula akajibiwa kuwa kuna wali na mshitakiwa akasema hataki
wali bali anataka ugali na mama akamjibu asingeweza kupika ugali na
kumsisitiza Siwema ale wali.
Zainab alisema baada ya majibizano hayo, mshitakiwa alimtukana matusi ya
nguoni mama yake, huku akisema hawezi kumzaa na kumkashifu kwamba hana
sehemu ya kumzalia huku akitishia kumwua akiahidi kumtoa roho ndipo
amjue yeye ni nani.
Kwa mujibu wa Zainab, alipoona ugomvi na matusi umezidi aliingia
chumbani mwake, na ndipo mlalamikaji akamfuata na kumtukana huku
akitishia kumwingilia kinyume cha maumbile.
“Baada ya hapo mshitakiwa alinivamia na kunidhalilisha kimaumbile kwa mikono yake,”alisema.
Baada ya ushahidi wa mama huyo dhidi ya Siwema, Mahakama ilitoa nafasi kwa kijana huyo kujitetea na Mahakama ikamtia hatiani.
Mwendesha mashitaka Blanka Shao alisema kwa kuwa japo mshitakiwa alikuwa
mkosaji wa mara ya kwanza, kitendo alichokifanya ni cha kifedhuli tena
haonyeshi kujutia, alishauri apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwake.
Hakimu Luanda alimhukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa kitendo alichomfanya mama yake mzazi.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 9 Ilala, mtaa wa Sophia Kawawa, nyumba namba 10.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA